Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MKURUGENZI wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhan amewataka watumishi wapya walioajiriwa katika halmashauri hiyo kutambua kuwa wanapotekeleza majukumu yao wanamuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan hivyo wawahudumie wananchi kwa uweledi.
Pia amewataka watumishi hao kutoa huduma kwa jamii kwa kuzingatia lugha ya staha kwa kuwaelewesha wananchi kuhusu huduma wanazozitoa badala ya kutumia jazba.
Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo leo tarehe 7 Machi, 2025 wakati akizungumza na watumishi hao wapya walioajiriwa katika halmashauri hiyo kwenye idara mbalimbali ikiwamo, afya, kilimo, sheria na fani nyingine.
“Naomba utambue popote unaposimama kama mtumishi wa umma, unasimama kwa niaba ya Mhe. Rais, ndio maana mwananchi akienda hospitali asipopatiwa matibabu ikitokea akakutana na kiongozi aliyepewa dhamana ya afya atamueleza kuwa hajapatiwa matibabu, kwa sababu kiongozi huyo pia anamuwakilishi Rais, hivyo lazima utambue huo umuhimu.
“Lakini pia ukiingia kwenye jamii hauingii na yale uliyotoka nayo darasani bali unakuwa na principal zako za kuwaelewesha wananchi wakuelewe, inabidi uwashawishi kwa kuangalia faida za pande zote ikiwamo za kiuchumi,” amesema.
Ametoa mfano kuwa fani kama vile wanasheria na madaktari ndio wanaotumia zaidi ya asilimia 80 ya kile walichotoka nacho chuoni na kwenda kutumia kazini.
“Wengine ukienda kwenye jamii usiende mzimamzima lazima uisome jamii ipoje, ila mtu ili aweze kukielewa kitu lazima awe na akili timamu sio kumlazimisha. Ukimshawishi na kumuelekeza na akakuelewa, hata ukitoka ataendelea kutumia kile ulichomuelekeza,” amesema.
Naye Ofisa Utumishi wa halmahauri hiyo, Henry Sadatale naye amewataka watumishi hao wapya kutambua kuwa malalamiko yoyote yatakayojiri kuhusu watumishi hao tafsiri yake wanaichafua ofisi wanayoitumikia.
“Kuna suala la matumizi ya lugha kwa sababu unaweza kupata jazba… lakini ukimjibu mtu vibaya hiyo ni tofauti na dhamira ya serikali, maana yake ni kwamba umeitukanisha serikali.
“Utoaji huduma lazima uzingatie staha, akija mgonjwa hata lugha tu inamponya. Pia kuna suala la kutunza siri, ni vema kutunza siri kwa sababu badala ya kuwa msuluhishi wa kila jambo unaweza kuleta mtafaruku ambao utaiharibu taswira ya ofisi yako,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa