MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani ameagiza kitengo cha lishe katika halmashauri hiyo kuandaa program maalumu ya upandaji wa miti ya matunda katika kila shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo ili kuwezesha wanafunzi kupata virutubisho mbalimbali ndani ya eneo lao la shule.
Pia ameagiza kitengo hicho kuandaa mpango wa uelimishaji wa mlo kamili kwa jamii zinazokabiliwa na utapiamlo kwa watoto wao ili kuepukana na vifo vinavyozuilika.
Mkurugenzi huyo ametoa maagizo hayo leo tarehe 3 Januari 2025 wilayani Magu mkoani Mwanza katika kikao maalumu kilicholenga kujadili Mapendekezo ya Rasimu ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kamati ya lishe ya wilaya.
Amesema katika shule nyingi, mpango wa upandaji wa mbogamboga umeonekana kuwa changamoto katika usimamizi na ustawishaji wa mbogamboga lakini kwa upande wa matunda ni rahisi kwa walimu na wanafunzi kuusimamia katika maeneo yao ya shule.
Aidha, ameagiza pia mpango huo uende sambamba na upandaji wa viazi lishe ili vitumike kuwapatia wanafunzi vitamini na virutubisho muhimu pindi wawapo shuleni.
Akizungumza baada ya kuwasilisha mapendekezio hayo, Afisa Lishe wa Wilaya hiyo, Magdalena Lema aliahidi kutekeleza ipasavyo maagizo hayo ili kuendelea kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa kuwapatia watoto wao lishe kamili itakayowafanya wakue vizuri.
“Kwa sababu kuna wazazi wengine wanavuna mazao shambani kwao mfano matunda kama mapapai na mengine lakini wanaleta sokoni na kuyauza yote bila kuacha machache kwa ajili ya matumizi ya watoto wao. Vivyo hivyo katika kundi la protini, wilaya yetu inaongoza kwa uvunaji na ulaji wa samaki lakini bado kuna watoto wenye utapiamlo,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa