MKUU wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari ametoa muda wa siku nne kwa watendaji wa kata na waratibu wa elimu kata kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, wanaripoti katika shule walizopangiwa.
Nassari ametoa maagizo hayo leo Alhamisi wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya wilaya hiyo (DCC) ambayo pamoja na mambo mengine imepitia na kujadili rasimu ya mpango na bajeti ya halmashauri kwa mwaka 2025/2026.
Amesema katika baadhi ya shule alizozikagua amebaini idadi ya wanafunzi walioripoti katika shule walizopangiwa hairidhishi.
“Hii karne ya 21, nasisitiza tena kila mtu atimize wajibu wake…nataka kila mtendaji wa kata aniletee orodha ya wanafunzi ambao hawajaripoti na mratibu wa elimu ya kata naye aniambie kwanini hajaripoti.
“Hadi kufikia tarehe 27 wiki ijayo nataka tufuatilie kila mwanafunzi iwapo ameripoti au hajaripoti na kama hajaripoti ni kwanini,” amesema.
Amesema namba za wanafunzi wanaoripoti kidato cha kwanza bado hazijaridhisha ilihali Serikali imejenga madarasa, kuboresha miundombinu ya ufundishaji pamoja na kuajiri walimu lakini cha ajabu wazazi wameshindwa kuhakikisha Watoto wao wanaripoti shuleni.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa