Jamii imetakiwa kujitoa kwa moyo wa kupenda kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji maalum ikiwemo watoto waishio kwenye mazingira magumu ambao ni yatima na wenye ulemavu.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 17, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Joshua Nassari wakati wa zoezi la kukabidhi misaada mbalimbali katika shule ya msingi Itumbili kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum lililoandaliwa na umoja wa madereva vijana Wilaya ya Magu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya muungano.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo DC Nassari amesema kuwa ni vyema jamii kwa ujumla kukumbuka kuwasaidia watoto ambao wana uhitaji kwani hata kwenye vitabu vya Mungu vimeendelea kuelekeza kutoa msaada kwa yatima,wajane na wale ambao hawajiwezi kwani kufanya hivyo ni kumpendaza Mungu.
Aidha aliwapongeza walimu wa wanafunzi wenye uhitaji maalum katika shule ya msingi Itumbili kwa kazi kubwa ya kuwafundisha wanafunzi hao na kuwataka kuwa na moyo wa uzalendo kwa kujitolea kufundisha elimu hiyo muhimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amesema madereva wana mchango mkubwa katika kuimarisha na kukuza uchumi hivyo wana wajibu mkubwa wa kufanya kazi zao kwa weledi ili kuepusha madhara kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa madereva vijana Wilaya ya Magu amesema wametoa misaada hiyo ikiwa sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya muungano ambao umekua ukisisitiza upendo katika jamii .
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa