MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Joshua Nassari ameongoza kikao cha maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kilichofanyika jana tarehe 20 Mei, 2025 wilayani humo na kusisitiza waratibu kujipanga ili Magu iibuke kinara katika ukaguzi wa miradi na maandalizi ya mbio hizo.
Hayo yanajiri baada ya wilaya ya Magu kushika nafasi ya pili kimkoa katika mbio za Mwenge huo wa Uhuru mwaka jana 2024.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi mbalimbali wa wilaya, akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Magu, Mohamed Ramadhani, Katibu Tawala Wilaya, Jubilate Lawuo, viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, watendaji wa kata, wakuu wa idara na wakuu wa taasisi za umma.
Wengine ni Waratibu wa Mwenge wa Uhuru ki-wilaya, Maafisa Uchaguzi, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Pamoja na mambo mengine watendaji wa kata walioratibu vema maandalizi ya mbio za mwenge mwaka jana na kutumiza malengo yao kwa zaidi ya asilimia 100 walipewa zawadi za cheti.
Mwenge wa Uhuru 2025 una kaulimbiu isemayo: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha ushiriki mpana wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia, huku amani na utulivu vikitajwa kuwa nguzo muhimu za maendeleo ya taifa.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa