MKUU wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amepongeza kazi nzuri ya malezi ya watoto inayofanywa na Shirika la Mavuno Village pamoja na JBFC yaliyopo katika Kijiji cha Kitongosima kata ya Kitongosima wilayani Magu mkoani Mwanza na kuahidi ushirikiano kwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali.
DC Nassari ametoa ahadi hiyo tarehe 10 Desemba mwaka huu wiayani Magu baada ya kutembelea vituo hivyo vinavyolea watoto yatima na wale walio katika mazingira hatari na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika makazi yao.
Mbali na kujionea shughuli za kiuchumi zinazozalishwa na watoto hao, shule wanazosoma pia amepongeza mfumo wa malezi unaotumiwa na Shirika la Mavuno Village kwa kuwale Watoto hao kwa mfumo wa kifamilia hali ambayo inawaondoa katika dhana ya uyatima.
“Lakini hii kitu mnayofanya humu ndani ikiwamo ufugaji, kilimo kiujumla life skills, isibaki humu ndani kwenu peke yenu, ni vizuri pia kuwafundisha na jamii inayowazunguka,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Awali akisoma risala ya kwa mkuu wa wilaya, Mkurugenzi wa shirika la Mavuno Village, Daniel Tanner alisema shirika hilo lililosajiliwa nchini mwaka 2004, linalea watoto zaidi ya 55 kwa mfumo wa familia ambazo hadi sasa wamefanikiwa kujenga nyumba na kutengeneza familia tano kati ya 20 wanazolenga kutengeneza.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la JBFC, Jonas Mwenda alisema shirika hilo mbali na kutoa malezi kwa watoto hao, pia linawapatia elimu ya msingi na sekondari katika eneo hilo huku mmoja wa watoto hao waliohitimu elimu ya juu akiajiriwa katika shirika hilo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa