Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutoa huduma za afya kwa ajili ya kupata dozi ya pili ya chanjo ya sindano ya Polio (IPV2) inayotarajiwa kutolewa wilayani hapa kuanzia tarehe 01 Mei 2025.
DC Nassari ametoa wito huo leo tarehe 30 Aprili, 2025 wakati akiongoza kikao cha kamati ya afya ya msingi Wilaya ya Magu ambacho kililenga kutoa elimu juu ya ugonjwa wa Polio ikiwemo chanzo chake, dalili, athari na njia za kinga, pamoja na kueleza jukumu la Kamati za Afya za Msingi katika kuhakikisha jamii inapata huduma ya chanjo kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Simon Mpandalume amewataka madiwani waliohudhuria kikao cha kamati ya afya ya msingi kwenda kutoa elimu ya chanjo hiyo kwa wananchi ili kujenga uelewa wa chanjo hiyo kwa wananchi.
Naye Diwani wa Kata ya Bukandwe, Marco Minzi ameshauri kuwepo na vituo katika vijiji ili kuwafikia wananchi wengi na kusaidia wananchi kutembea umbali mrefu kufata huduma za chanjo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa