Mkuu wa wilaya ya Magu Dr. Philemon Sengati (PhD), leo tarehe 02.06.2020 amezindua rasmi ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari kijiji cha salama-Bugatu inayojengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya “Alliance Ginnery” inajishughulisha na ununuzi na uchakataji wa zao la Pamba iliyoko katika kijiji cha Kasori Wilaya ya Bariadi Mkoani –Simiyu.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amewasili mapema katika Kiijiji cha Bugatu akiwa ameongozana na kamati ya Ulinzi na Usalama , Mkurugenzi Mtendaji (W), Katibu wa CCM (W), na kupokelewa na maandamo ya mamia ya wananchi wa Kata ya Ng’haya, wakiimba nyimbo za pongezi kwa Serikali iliyodhamiria kwa dhati kuleta maendeleo dhahiri wakionesha kuvutiwa na utendaji bora wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Jemedari mkuu Dr. John Pombe Magufuli Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Meneja wa Kampuni ya “Alliance Ginnery” Ndugu Boaz Ogola, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe. Boniventura Kiswaga, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Lutengano Mwalwiba na Diwani wa Kata ya Ng’haya Gerald Paul kupitia vikao mbalimbali waliomba Kampuni kufadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya pili katika Kata ya Ng’haya ambapo watoto wamekuwa wakisafiri umbali mrefu. “Sasa kampuni imekubali na Mhe: Mkuu wa Wilaya tunakuhakikishia kuwa tunajenga shule hii kwa ubora na kasi kama ilivyo kasi ya Chama Cha Mapinduzi kuleta maendeleo nakuahidi tutakukabidhi Vyumba vinne vya madarasa,jengo la utawala na vyoo matundu kumi. Hii ni kwa muda wa miezi miwili tu”. Amesisitiza Ogola –Meneja wa Alliance Ginnery.
DC. Sengati ameishukuru na kuipongeza Kampuni ya Alliance Ginnery kuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo ambaye amejipambanua na anajitambua kwa kuungana na jamii pamoja na Serikali katika shughuli za maendeleo ya jamii. Hivyo basi sura na mwonekano wa wananchi kisaikolojia wamehamasika na mradi huu naamini wako tayari na wako kushiriki kikamilifu.
“Wafadhili wetu mko katika mikono salama na ninawataka wananchi wote kuwa walinzi na washiriki katika kufanikisha malengo yetu ya kuwaokomboa watoto wetu waliokuwa wakipata shida ya kutembea umbali mrefu km 16 kutoka Salama hadi Ng’haya. Aidha Mhe: Mkuu wa Wilaya amewataka watanzania kujivunia Uongozi wa Rais Magufuli ambao Dunia na Ulimwengu unamheshimu na kumtumainia kama Dira kwa Viongozi wa Dunia na Mzalendo namba moja anayelinda utu, haki na maslahi ya Watanzania na Waafrika kwa ujumla. Pia Mheshimiwa DC amekabidhi mchoro wa ramani ya majengo ya Shule kwa mfadhili na kuwaahidi wananchi kuwa mradi utasimamiwa kwa taratibu zote za Kiserikali na utakuwa mradi wa mfano katika shule zote za Magu.
Dominique Bubeshi Mwakilishi wa Mbunge katika hafla hiyo amesema kuwa Mbunge wa Jimbo la Magu ana imani kubwa na Uongozi wa DC Sengati kuwa ni kiongozi anayeishi maneno yake na kuwa ni mahiri katika wa uhamasishaji na uchangiaji wa maendeleo jimboni.
Afisa Tarafa ya Ndagalu Bi.Grace Msilanga amesema kuwa hii ni ndoto ya muda mrefu ya wananchi ambayo DC Sengati ameitimiza kwa wakati.
Gerald Paul Diwani wa wakati wa Ng’haya amesema kuwa mradi huo ni wa Kata ya Ng’haya hivyo wananchi waupokee na washiriki kikamilifu kadri watavyoombwa kushiriki kwa namna yoyote, “Mimi siyo msemaji bali Mtendaji” Amesema Gerald Diwani wa kata ya Ng’haya.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa