Mkuu wa Wilaya ya Magu Mheshimiwa Salum Kalli tarehe 23.10.2020 amekabidhi fedha na pikipiki 21 kwa vikundi vya wajasiliamali (wanawake Vijana na walemavu), Maafisa Ugani na polisi kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayorejeshwa kwa wananchi.
DC Magu amempongeza Mkurugenzi Mtendaji (W) na timu yake kwa kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na walemavu “ Hongereni sana kwa kazi mnzaozifanya na muendelee na ushirikiano huo, mimi nimefarijika sana yanayofanyika katika Taifa hili ni makubwa sana kwani Rais Wetu amejipambanua sana katika kuwaletea wananchi maendeleo. Tutawapatia jumla ya pikipiki 21 leo, mkazifanyie kazi iliyikusudiwa na mfikie watu kwa wakati na fedha hizo mlizopewa mkazisimamie vizuri ili ziwe na tija na kuwasaidia” amesema DC Kalli.
Kabla makabidhiano Hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Magu Ndugu. Lutengano George Mwalwiba amesema kuwa kwa Mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo kiasi Tshs 210,000,000 kwenye vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo imetolewa kwa asilimia 100. “kwa Mwaka huu robo ya kwanza pekee tumekopesha vikundi kiasi cha Tshs. 90,000,000”. Amesema kuwa Halmashauri inategemea mapato yake ya ndani kwa 64% kutoka sekta za kilimo na mifugo ndio maana Menejimenti imeamua kutoa pikipiki 10 kwa Maafisa Ugani. “kwa miaka miwili mfululizo tumekuwa vinara kwenye maonyesho ya wakulima nanenane kanda ya ziwa Magharibi” amesema Lutengano.
Aidha amepongeza kamati ya ulinzi na usalama kwa ushirikiano inaotoa katika kuhakikisha Halmashauri inakusanya Mapato yake na kutokana na mapato hayo Halmashauri imetoa pikipiki 3 kwa Jeshi la Polisi Magu ili ziweze kurahisisha utendaji kazi, kompyuta mpakato 1 katika Ofisi ya TAKUKURU na Ofisi ya Usalama Kompyuta Mpakato 1. Vikundi vya vijana vimepata pikipiki 8 kwa ajili ya uzalishaji.
Wajasiriamali wameshukuru sana kwa mikopo waliyoipata kutoka Halmashauri na wameahidi kushirikiana na Serikali hii ya wamu ya Tano ya Dkt John Pombe Magufuli. Nao Maafisa Ugani wametoa shukrani na kuahidi kuwa wamejipanga kufanya uhamasishaji wa kilimo nyumba kwa nyumba na kijiji kwa kijiji.
Kwa niaba ya Kamati ya ulinzi na usalama OCD Magu Ndugu Mahamoud Banga ameshukuru mkurugenzi na timu yake ya Menejimenti kwa kutoa pikipiki 3 kwa Jeshi la Polisi na Kompyuta Mpakato kwenye Ofisi za usalama na TAKUKURU. Amesema pikipiki zitapelekwa kwenye vituo vya polisi kama ilivyopangwa. Aidha amesema Kaulimbiu ya Kamati ya Ulinzi na usalama Magu inasema “umoja wetu ndiyo Nguvu yetu na nguvu yetu ndiyo umoja wetu”
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa