Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt. Philemon Sengati ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama (W) ametangaza kufuta Chama kinachodaiwa kuwa ni cha kutetea Wafugaji katika kijiji cha Kisamba Wilayani Magu. Amefikia uamuzi huo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 13.11.2018 alipofika katika kijiji hicho kwa lengo la kusikiliza chanzo cha mgogoro uliodumu kwa miaka sita sasa, akiwa katika mkutano huo amehoji uwepo wa wafugaji na chama chao ambacho siku chache alifanya nao kikao Ofisini kwake.
Viongozi hao wa wafugaji hawakufika katika mkutano huo muhimu uliolenga kutatua mgogoro ambao unatishia amani na usalama kwa Wananchi. Kufuatia kupuuza huko amemhoji Mkurugenzi Mtendaji iwapo Chama hicho kinatambulika kisheria majibu yakawa kuwa hawana chama cha wafugaji na hawajawahi kusajiliwa katika Halmshauri ya Magu. Ndipo Mkuu wa Wilaya akatangaza kukifuta chama hicho na kumwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya kuwafikisha Ofisini kwake waliokuwa wakijinasibu kuwa ni Viongozi wa Chama Cha Wafugaji ili wajieleze kwani nini wamejivika majukumu hayo kinyume cha sheria.
Mkuu wa Wilaya ameongozana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Magu, Pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya aliyewakilishwa na Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya mji mdogo wa Magu pamoja na Diwani wa kata ya Lubugu Mheshimiwa Lucas Zabron. Wananchi wamelalamikia kijiji chao kuvamiwa na Wafugaji wenye makundi makubwa ya mifugo ambayo inaharibu mazao ya wakulima kila kukicha na jambo hili limepelekea kuibuka chuki kwa baadhi ya Wakulima wanaoharibiwa mazao yao na kushambuliwa na wachungaji kwa kupigwa na kujeruhiwa.
Vilevile wananchi wamemweleza Mkuu wa Wilaya kuwa Viongozi wa Serikali ya Kijiji wamekuwa vinara wa mgogoro huo kwani huwakaribisha wafugaji na hupatiwa kitu kidogo, na hii ndiyo sababu Wafugaji wamekuwa na kiburi wanadiriki kuchungia katika mashamba ya mazao ya wakulima hata nyakati za usiku, pia wamekuwa na majibu ya kejeli kuwa watakaoendelea kuhoji mifugo katika kijiji hicho wataozea jela, Pia Umoja wao huo ni wa Wafugaji wavamizi lakini wafugaji wenyeji hawashirikishwi katika hicho chama, ndiyo maana hata leo Mheshimiwa DC hawapo katika mkutano wako. Amesema mmoja wa wanakijiji anayedai kuwa ni mhanga wa sakata hilo.
DC Sengati akiwahutubia wananchi hao amewaaambia kuwa anahitaji kuiona Kisamba ikiwa na amani tena amani ya kudumu bila mgogoro, na kwamba sifa ya kuwa na mgogoro wa muda mrefu ni jambo lisilokubalika katika kipindi hiki tunapojielekeza katika ujenzi wa Magu ya mfano Tanzania katika shughuli za kimaendeleo. Pia “Rushwa ni jambo ambalo halina nafasi katika Wilaya ya Magu.
Pia Viongozi wote tubadilike tutangulize maslahi mapana ya Taifa mbele na siyo maslahi binafsi au kikundi chochote kile hata kama ni cha Matajiri, Sisi tunatekeleza ndoto za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwatetea wanyonge na kuhakikisha haki na usawa vinastawi katika Taifa letu. “Niwaalike kwa namna ya pekee kujiepusha na rushwa inayozalisha migogoro kwa uporaji wa haki za wengi,
Mimi sikuja magu kutafuta utajiri hutosikia kuwa nimepokea wala kuomba rushwa. Mwenyekiti wa Kijiji na Serikali yako umetajwa kujihusisha na rushwa ambayo ndiyo kiini cha mgogoro huu tutakuchunguza na kesho saa 2:00 asubuhi ufike Ofisini kwangu na wananchi endeleeni kutupatia ushirikiano na taarifa sahihi kwa kila hatua ili tuweze kuondosha mgogoro huu na kuanzia leo ni maarufuku kwa mfugaji yoyote yule, Kulisha, Kuharibu mazao, kutishia na kuwashambulia wakulima”.
“Pia nakuomba Mkurugenzi wa Wilaya Shughulikieni suala la kuwabaini wafugaji wenye makundi makubwa ya mifugo walivamia na namna walivyoingia, "pia muone namna ya kutenga maeneo ya malisho na mashamba ili atakayeingilia eneo la mwingine sasa tuweze kuanza naye kumshughulikia” amesema Dkt Sengati.
.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji akipokea maagizo ya Mheshimiwa DC amesema kuwa ‘ “Tumepokea lakini wananchi mnajua namna mlivyoasisi mgogoro huu, maana wafugaji hawawezi kuja bila ninyi kuwakaribisha, Kwa hiyo tutaona namna bora ni kuwashirikisha wote katika maamuzi, kuondosha hili balaa la Wakulima kulishiwa mazao yao kwa kweli inarudisha nyuma maendeleo yenu wakulima” Amesema Fundikira kwa niaba ya mkurugenzi Mtendaji wilaya.
Magu Kusema na Kutenda.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa