MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amekutana na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wilayani humo ambao pamoja na mambo mengine wamemhakikishia ushirikiano katika kuwafikishia maendeleo wananchi na kudumisha amani.
DC Lawuo amekutana na viongozi hao wa vyama vya siasa leo Jumatatu tarehe 18 Agosti, 2025 mjini Magu na kuwasisitiza kudumisha amani hususani katika kipindi hiki cha mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.
“Nimefurahi kukutana nanyi ndugu zangu ili kuendelea kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu wilaya yetu lakini kubwa ni kuomba uendelevu wa ushirikiano wenu katika kutekeleza miradi ya maendeleo lakini pia kudumisha amani katika jambo kubwa la uchaguzi mkuu,” amesema DC Lawuo.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Katibu wa Chauma wilaya ya Magu, Juma Nziajose mbali na kupongeza Lawuo kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan amempandisha kuwa mkuu wa wilaya hiyo kutoka kuwa Katibu tawala, amemhakikishia kuwa wataenda kuwa mabalozi wa amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.
“Ni kweli kabisa asilimia 90 ya watu wanaoweza kuvuruga amani ni viongozi wa vyama vya siasa, sisi tunakudhibitishia kuwa hilo hapa Magu halitatokea kamwe kwa sababu tunakufahamu tangu ukiwa DAS hapa umetupa ushirikiano wa kutosha, umetusikiliza na kutupa faraja pale tulipokwama hivyo usiwe na wasiwasi.
Naye Katibu wa ACT Wazalendo, Robert Busumabu pia alimuomba mkuu huyo wa wilaya kuendeleza ushirikiano na wananchi wa Magu pamoja na makundi mbalimbali ili kuboresha mahusiano yaliyopo
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa