-Mamia wafika kujionea na kupata elimu ya ufugaji
MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo ametembelea banda la Halmashauri ya wilaya hiyo katika maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza na kupongeza teknolojia za kisasa zilizoletwa na wataalamu wa wilaya hiyo kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi.
DC Lawuo alitembelea banda la halmashauri ya Magu jana Agosti 3, 2025 na kuelekeza kuridhishwa na maandalizi kabambe yaliyofanywa na wataalam wa sekta hiyo hususani katika utoaji elimu kwa wafugaji, wavuvi na wakulima.
Katika maonesho hayo ambayo yalianza Agosti Mosi, wananchi wamekuwa wakifurika katika banda la Magu kujionea teknolojia mbalimbali za ufugaji wa samaki pamoja na vifaranga wake, ufugaji wa mifugo mbalimbali ya kisasa pamoja na kilimo cha umwagiliaji kama vile uandaaji wa mbegu bora za mpunga.
Januari Simba ambaye ni mtaalamu wa ufugaji na uvuvi wa samaki amemueleza mkuu wa wilaya hiyo pamoja na wananchi waliofika bandani hapo namna walivyobuni teknolojia ya kisasa ya kuangua vifaranga wa samaki pamoja na ufugaji wa samaki aina ya sato katika mabwawa madogo kwenye makazi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo anayeshughulikia kilimo cha umwagiliaji hususani mpunga, Zawadi Madoshi naye amewakaribisha wananchi kwenda kujifunza namna ya kutumia teknolojia ya maji, chumvi na yai kupata mbegu bora ya mpunga.
Nanenane 2025 imekuja na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa