Taasisi isiyo ya kiserikali ya Determined Education and Rural Empowerment (DERE) imekabidhi msaada wa viti mwendo 75 kwa Halmashauri mbalimbali za mkoa Mwanza ambapo wilaya ya Magu imenufaika kwa kupata viti 13 vitakavyotolewa kwa wanafunzi na watu wazima wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Akizungumza katika hafla ya kupokea viti mwendo hivyo iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Devine Hope , Bujora, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Jubilate Lawuo, aliipongeza taasisi hiyo kwa moyo wa upendo waliouonesha kwa watu wenye mahitaji maalum.
Amesema msaada huo utasaidia katika kurahisisha harakati za kila siku za wanafunzi na watu wazima wenye mahitaji maalum, hususan katika kupata elimu, huduma za afya na ushiriki wa kijamii.
Aidha, DC Lawuo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau wengine, mashirika ya kiraia, watu binafsi na taasisi mbalimbali kuiga mfano huo kwa kusaidia makundi yenye uhitaji.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa