Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani wamezindua zoezi la uandikishaji wananchi katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kujiandikisha katika vitongoji wanavyoishi.
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo tarehe 11 Oktoba mjini Magu mkoani Mwanza, Nassari amejiandikisha katika kituo cha Unyamwezini kilichopo kata ya Itumbili huku Mkurugenzi wa halmashauri hiyo akijiandikisha katika kitongoji cha National kilichopo kata ya Magu Mjini.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa sababu ni zoezi ambalo linafanyika chini ya dakika moja.
“Uandikishaji huu hauna complication (vikwazo) ndani ya dakika moja unajiandikisha kisha unaendelea na majukumu yako pia kuna mawakala wa vyama vyote, usalama na amani ipo ya kutosha.
“Mara nyingi watu wanadhani uchaguzi ni ule wa uchaguzi mkuu tu, lakini huu ni muhimu zaidi kwa sababu hawa ni viongozi ambao wapo na wewe usiku na mchana, ndio viongozi ambao kwa lolote nyumbani kwako anakuwa wa kwanza kufika,” amesema Nassari.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo amesema ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha kwa sababu zoezi hilo halihitaji mwananchi kuja na kitambulisho chochote zaidi ya majina kamili kwani wakala anaweza kutambua mkazi wa kitongoji husika.
“Wengine wanasema tayari walijiandikisha mwezi uliopita, ule ulikuwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, na baada ya kujiandikisha orodha itabandikwa kwenye maeneo yote ya wazi hivyo wananchi waende kuhakiki au wale ambao hawastahili kupiga kura waweze kutolewa kisha tuende kwenye awamu nyingine ya uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali,” amesema.
Aidha, baadhi ya mawakala wa vyama vya siasa akiwemo Philemon John (Chadema) na Fausta Anthoni (CCM), wamesema zoezi hilo linafanyika kwa usalama hivyo wananchi wajitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwa na sifa za kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Uzinduzi wa zoezi hilo la uandikishaji ambalo litafanyika kwa siku 10 kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu, limeenda sambamba na shamrashamra za maandamano yaliyoanzia katika ofisi za wilaya ya Magu hadi uwanja wa Mwanankanda ambako kumefanyika mchezo wa soka kati ya mashabiki wa Simba na Yanga.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa