Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt. Philemon Sengati ametoa shukrani hizo katika siku ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika katika uwanja wa Sabasaba tarehe 13.12.2018. Amesema ” napenda kuwashukuru sana kwa kuhusianisha suala la Ukatili wa Kijinsia na zoezi tulilolifanya la usafi wa mazingira kwa mji wetu wa Magu. Nawapongeza sana wote kwa ushiriki wenu na kuweza kufanikisha siku hii ya leo kuwa pamoja kwa wingi kiasi hiki”.
Aidha amesema Siku hii ya Kupinga ukatili wa Kijinsia Duniani ni siku ya kutafakari kujua ukatili wa kijinsia ni nini, unafanyika vipi, ni nini madhara yake na namna ya kuzuia ukatili huo usiendelee. Serikali yetu kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali itaendelea kuongeza juhudi za kuwezesha suala la utoaji wa Elimu katika maeneo yote ya Nchi hususani Vijijini. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “FUNGUKA, PINGA UKATILI WA KIJINSIA, ELIMU SALAMA KWA WOTE”.
“Magu kama zilivyo wilaya nyingine nchini ni miongoni mwa Wilaya zinazokabiliwa na Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia miongoni mwa Wananchi kwa kiasi kikubwa. Ukatili huu unaosababisha Madhara mengi kwenye Jamii kiuchumi na Kiafya. Aidha kuna aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia kama vile kimwili, Kingono, Kiuchumi na Kiakili/Kisaikolojia” amesema Dkt. Sengati.
Amewaomba Wananchi kutoa ushirikiano kuondoa aina zote za ukatili wa kijinsia na kufikia usawa wa kijinsia ili kuwa na jamii iliyo salama na yenye ustawi. “Hivyo ninawataka wanajamii wote, viongozi wa Madhebu ya Dini na Watendaji wote wa Serikali, kwa ujumla wetu kuhakikisha tunadhibiti vitendo vyote vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika Jamii. Hii ikiwa ni pamoja na kuripoti matukio yote ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanayotokea katika jamii na kuhakikisha tunatoa ushahidi pindi tukihitajika. Kwa kufanya hivyo tunaweza kuongeza umri wa kuishi wa watu wetu hivyo kuchangia kwa ukamilifu ujenzi wa Taifa.
Mwisho, amewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kuisaidia Halmashauri yetu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ambapo amewasisitiza wananchi kuendelea kuifanyia kazi Kauli mbiu ya mwaka huu ya “FUNGUKA, PINGA UKATILI WA KIJINSIA, ELIMU SALAMA KWA WOTE”. Kwa pamoja tunaweza kuzuia ukatili wa kijinsia, tuungane na kuendeleza nchi yetu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa