Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Magu limeagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Magu kutekeleza miradi ya miundombinu ya barabara yenye changamoto kwa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo hayo zinatumika ipasavyo.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 15 Novemba 2024 na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Mpandalume katika Kikao cha Baraza la Madiwani robo ya kwanza kilichofanyika wilayani Magu ambapo Baraza hilo limepokea taarifa za utekelezaji wa Shughuli za maendeleo ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024.
Mwenyekiti huyo amesema madiwani wengi wamekuwa wakipiga kelele kuhusu kusuasua kwa miradi inayogusa taasisi hizo kwa kuwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wamepatikana bila hata kushirikisha mameneja wa wilaya katika taasisi hizo.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema hivi karibuni halmashauri kwa kushirikiana na jeshi la polisi litaanza kuwasaka wananchi ambao kaya zao hazina choo ili kudhibiti mlipuko wa kipindupindu ambao ulijitokeza katika tarafa ya Ndagalu.
Akikazia kuhusu mlipuko huo wa kipindupindu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani alisema baadhi ya kaya zimekuwa zikikaidi kwa makusudi kufuata maelekezo ya watalaam wa afya ambao wamekuwa wakitoa huduma, elimu na tiba kuhusu ugonjwa huo na matokeo yake, mgonjwa katika familia akipona baada ya siku chache anapokelewa tena mgonjwa toka kwenye familia ile ile kwa ugonjwa ule ule. Ukifanyika ufuatiliaji ngazi ya familia wataalam hukuta dawa za kutibu maji familia hawazitumii, hawachemshi maji na maji tiririka hayatumiki katika familia hizo.
“Tumezuia mikusanyiko yote hadi minada hakuna chakula kinachouzwa sio hali nzuri lakini inasababishwa na baadhi ya wananchi ambao hawana vyoo na wanaendelea kuwa chanzo cha kusambaza vimelea vya kipindupindu.
“Watu wana nyumba zilizoezekwa bati za msauzi lakini eti hazina choo"
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa