Maafisa Ugani Wilaya ya Magu wametakiwa kutumia utaalamu wao kuwafikia wakulima wa zao la Pamba na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa cha zao hilo ili kufikia lengo la Serikali kuzalisha tani 500,000 kutoka tani 17,300 katika msimu wa 2022-2023.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Pamba nchini Tanzania Bwana Agrey Mwanri wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo wa zao la Pamba iliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Magu na kuwakutanisha Watendaji wa vijiji,Wenyeviti wa vijiji,Maafisa Ugani pamoja na baadhi ya Watumishi wa Serikali ngazi ya Halmashauri na Wilaya .
Akizungumza Wakati wa Semina hiyo, Bw. Mwanri amesema kuna haja ya kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa Wakulima wa zao hilo ili kuepukana na changamoto ya Wakulima kulima kiholela ambapo husababisha kuvuna nje ya matarajio.
" Viongozi wawe mfano katika zao hilo kwa kwa kufanya hivo kutainua na kuongeza pato la mtu mmoja na Taifa kwa ujumla " amesema Mwanri.
Aidha amewaasa Wakulima wa zao la Pamba kuzingatia masharti na kanuni za kilimo bora katika uzalishaji ili kulijengea thamani zao hilo na kujiongezea kipato cha mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda amewataka maafisa ugani kusimamia kanuni za kilimo kwenye maeneo yao ili kuendelea kuongeza thamani ya zao la pamba.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa