WIZARA ya Fedha kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu, leo Jumatatu imetoa mafunzo kuhusu mikopo kwa wana-vikundi vya kijamii, watoa huduma za kifedha na wana-ushirika kwa lengo la kuwapa elimu sahihi kuhusu ukopaji na ukopeshaji wa mikopo hiyo.
Katika mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Kyande wilayani Magu, jumla ya washiriki 176 wamenolewa kuhusu mikopo hiyo.
Akizungumza na washiriki hao, Kyande amewataka watoa huduma hizo za mikopo kuzingatia taratibu na sheria za mikopo ili kutowaumiza wakopaji kwa sababu lengo la Serikali ni kuona wananchi wanapiga hatua kimaendeleo.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapenda kuona wananchi wake wanapiga hatua kimaendeleo na sio kuingia kwenye mikopo hii ya nyonya damu ambayo kwa hakika inarudisha nyuma maendeleo ya wengi.
“Natoa rai kwenu washiriki kutumia elimu hii mnayoipata kutumia mikopo mnayoomba kwa ufanisi ili jamii ione umuhimu wa sekta hii ya fedha,” amesema.
Naye Mwezeshaji kutoka wizara ya fedha, Salim Halfan alianza kwa kuwaonya wakopaji kujiwekea malengo ya mikopo wanayokopa badala ya kuitumia kwa mambo yasiyofaa hali inayowaletea changamoto katika utekelezaji wa malengo ya mikopo yao.
“Unaweza kukuta mtu amekop 20,000 badala aitumie kwa malengo aliyodhamiria unakuta anajipoza kidogo kwa chips mayai, baada ya muda hela inaisha na hajui amefanyia nini mwisho wa siku anashindwa kurejesha mkopo na kuingiq matatizoni,” amesema na kusisitiza elimu kuhusu mikopo ni muhimu kwa jamii.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa