Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Sekta ya Biashara na Uwekezaji katika Wilaya ya Magu imepongezwa kwa kuboresha mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara hatua iliyochochea ongezeko la makusanyo ya mapato kutoka wafanyabiashara na wawekezaji wanaotumia fursa zilizopo kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara wilayani Magu (TNCC), Dominique Bubeshi wakati akichangia mjadala katika Kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya ya Magu kilichofanyika katika mjini Magu mkoani Mwanza.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wafanyabiashara wilayani Magu wamepewa ushirikiano wa kutosha kutoka na maofisa biashara na watalaam wengine wa halmashauri ya Magu hali iliyowafanya kuchangia mapato ya halmashauri kwa hiari na kwa kiwango cha kuridhisha.
Ametoa mfano katika kipindi cha mwaka 2021/2022 makusanyo ya leseni za biashara yalikuwa milioni 185.7 lakini hadi kufikia mwaka 2024/2025 mapato hayo yamefikia milioni 300.4
“Pia sasa hali ni tofauti kwani wafanyabiashara wakisikia maofisa biashara kutoka halmashauri wanaenda kuwatembelea, hawakimbii tena na kufunga fremu zao, kwa sababu wametengeneza mazingira rafiki ya ukusanyaji mapato badala ya kufunga biashara,” amesema.
Awali akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo aliwasisitiza wajumbe wa baraza hilo kuendelea kutoa ushirikiano kwa maofisa wa halmashauri hiyo ili kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye wilaya ya Magu.
Naye Katibu wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani alisema ameanzisha kanda nne za ukusanyaji mapato ili kusaidia wananchi kupata huduma zinazopatikana katika ofisi kuu kwa urahisi.
Alitaja kanda hizo kuwa ni Kisesa, Nyanguge, Magu pamoja na Kabila ambapo zimesheheni watalaam mbalimbali watakaowapatia wananchi huduma muhimu ikiwamo matumizi ya mfumo Tausi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa