WENYEVITI wa vijiji na vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu wametakiwa kuzingatia maadili na uzalendo pindi wanapotekeza majukumu yao ili kujenga mazingira rafiki kati yao na wananchi wanaowahudumia.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa mjini Magu mkoani Mwanza na Katibu Tawala wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo wakati akifungua mafunzo kwa wenyeviti hao kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Nassari.
Wenyeviti hao wa vijiji 82 na vitongoji 508 wilayani Magu, ni wale waliochaguliwa katila uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana.
Akizungumza na washiriki hao, Lawuo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wenyeviti hao kuwa imara katika nafasi zao za uongozi na kuwa mfano bora wa kuigwa kwa uweledi na wananchi wao.
“Kiongozi bora unatakiwa kuzingatia maadili, hatutaki kusikia mwenyekiti analalamikiwa na wananchi kwa kuharibu ndoa za watu au kuharibu ndoto za wasichana wadogo, tunaamini Magu haya hayapo hivyo mafunzo mnayopewa tunataka mkayazingatie,” amesema.
Pamoja na mambo mengine amewataka viongozi hao kutokuwa sehemu ya migogoro ya ardhi ambayo katika siku za karibuni imeshika kasi wilayani humo.
“Pia tunawataka muwe walinzi wa usalama katika maeneo yenu, badala ya kujimwambafai mnatakiwa kuwa watatuzi wa migogoro katika maeneo yenu,” amesema.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, Ofisa Utumishi wa wilaya hiyo, Henry Sadatale amesema mafunzo hayo ambayo yanafanyika katika halmashauri zote za mkoa wa Mwanza yanalenga kuwapatia maarifa na elimu viongozi hao katika kutekeleza majukumu yao kwa urahisi.
Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Hombolo, Dk. Muhsin Danga amewataka viongozi hao kuwa na hekima na busara huku wakifanyaka kazi zao kwa kutozingatia mihemko.
Mmoja wa wenyeviti hao kutoka Kitongoji Ngalasani Kijiji cha Nsola, Ramadhani Philipo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi ili kuwa kioo kwa jamii anayoiongoza.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa