Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu tarehe 16.08.2018 ambapo ametembelea mradi mkubwa wa maji Magu Mjini na mradi wa kisima kirefu kinachotumia Mfumo wa Jua (Solar) Katika kijiji cha Lubugu. Amesema kwamba, Halmashauri ya wilaya ya Magu imekuwa na changamoto ya ukosefu wa maji ya kutosha kwa muda mrefu ambapo hadi sasa upatikanaji wa maji ni asilimia 23 maeneo ya mjini na asilimia 45 maeneo ya vijijini. “Hivyo Serikali imeleta mradi huu Mkubwa wa maji pindi utakapokamilika tatizo la maji Magu litakwisha, na mradi huu utagharimu Fedha za kitanzania Billioni 12” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha ameagiza Mkandarasi kukamilisha Mradi huo mkubwa wa maji kufikia Mwezi Februari 2019, japo mkataba unaonyesha mradi utakamilika mwezi Mei, 2019. ”Msimamizi wa Mradi (Consultant) asimamie Mkandarasi masaa 24 kwa siku ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wapate huduma ya maji”.
Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe. Destery Kiswaga amesema kwamba, ifikapo Mwaka 2019 suala la maji litakuwa historia kwani huu ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015. “Chanzo cha Maji kilichopo hakiwezi kutosheleza wananchi wote kwa sasa kwani idadi ya watu imeongezeka, mradi uliopo ulijengwa mwaka 1974 pindi watu wakiwa 6000 tu, hivyo wananchi waendelee kuamini Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania iliyopo Madarakani inayopenda maendeleo Wananchi wake chini ya Dkt. John Pombe Magufuli” amesema Kiswaga.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt. Philemon Sengati amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteuwa kuwa mwakilishi wake katika Wilaya ya Magu ambapo, ameahidi kufuatilia shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kuhakikisha zinafanyika kwa ufasaha. “Mradi huu mkubwa wa maji utakuwa wa Kihistoria kwani ukikamilika utawaondolea wananchi adha ya maji katika wilaya ya Magu”
Pamoja na mradi huo mkubwa wa maji, Mheshimiwa waziri Prof. Mbarawa ameweka jiwe la ufunguzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Lubugu. Amesema kwamba, nia ya Serikali ni kupeleka maji kila eneo la nchi hii hivyo kwa kutambua hilo “Serikali imeamua kujenga mradi huu wa maji unaotumia mfumo wa jua (solar) katika kijiji hichi, hivyo mtumie maji haya na kuulinda mradi huu uendelee kufanya kazi muda mrefu kwani umegharimu kiasi cha fedha shilingi Millioni 193, pia ni mradi wa gharama nafuu katika uendeshaji wake” amesema Prof. Mbarawa. Aidha, ameahidi kufanyia kazi suala kupeleka mradi wa maji wa kutumia mfumo wa Jua katika kijiji cha Sayaka.
Mhe. Waziri wa Maji na Umwagiliaji akipata Maelezo Juu ya utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji Magu Mjini
Mhe. Waziri wa Maji na Umwagiliaji akikagua ujenzi wa Mradi wa Maji Magu Mjini
Mhe. Waziri wa Maji na umwagiliaji akichimba Mtaro wa kupitisha bomba la maji
Kaimu Mhandisi wa Maji Magu akieleza Juu ya Mradi wa Kisima Cha kutumia Mfumo wa Jua (solar) Kijiji Cha Lubugu
Mbunge Jimbo la Magu akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Lubugu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Magu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lubugu
Mhe. Waziri wa Maji na Umwagiliaji akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Lubugu
Uzinduzi wa Mradi wa Kisima cha kutumia mfumo wa Jua (Solar) katika Kijiji Cha Lubugu
Mhe. Waziri wa Maji na Umwagiliaji akimtwisha maji Mwananchi Katika kijiji cha Lubugu baada ya uzinduzi wa Mradi huo
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa