Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, amekuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya miaka 50 ya makumbusho ya Wasukuma Bujora yaliyofanyika tarehe 03.06.2018. Akiwa katika maadhimisho hayo, amewashukuru Watemi wa Kisukuma kwa kusimamia makumbusho ambapo ameahidi kuwa, Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wa kuendeleza kituo hicho, pia amesema kila mwaka Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo lazima itakuwa inashiriki maadhimisho ya Wasukuma kwani makumbusho haya ni ya kiserikali.
Aidha, Mheshimiwa amefurahishwa na kaulimbiu ya maadhimisho ya makumbusho inayosema “Kazi ni Utamaduni Wetu”. Kutokana na kauli mbiu hiyo, Waziri amesema kazi ndio msingi wa kila kitu na “Taifa lisilo kuwa na Utamaduni, ni Taifa mfu. Taasisi ya Taifa ya sanaa ya Bagamoyo itafika hapa Bujora kuangalia namna ya kuboresha kituo cha makumbusho Bujora kwani kimeanza kuchakaa” amesema Dkt. Mwakyembe.
Pia, Dkt Mwakyembe ameahidi kuwasiliana na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili kuweka utaratibu wa kuanza kuonyesha kipindi cha ngoma zetu kila wiki. Kwa kuwa watalii wengi wanaokuja kutembelea kituo huwa wanalala Mwanza mjini, ameshauri Mkoa utoe ushirikiano wa kuboresha kituo hiki cha makumbusho cha Bujora.
Watemi wa Kisukuma wamemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli, kwa kukubali kujenga barabara ya Lami kutoka Barabara kuu iendayo Musoma hadi kituo cha Maonyesho Bujora kwani itasaidia wageni mbalimbali kwenda kuangalia na kujifunza utamaduni wa Kisukuma katika makumbusho hayo.
Baada ya hotuba yake, Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo amezindua tamasha la ngoma katika siku ya maadhimisho ya Makumbusho ya Wasukuma Bujora.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa