Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stagomena Tax leo Jumanne amejiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika kituo cha Unyamwezini kilichopo kata ya Itumbili wilaya Magu mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kupokewa na Mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari na kujiandikisha, Dk. Tax ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha na kufikia asilimia 44 ya lengo huku ikiwa ni kwa muda wa siku nne pekee.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa serikali za mitaa lililofunguliwa tarehe 11 Oktoba mwaka huu hadi tarehe 20 Oktoba ili kumchagua kiongozi atakayeungana na serikali kuwaletea maendeleo.
Amesema wananchi hawatakiwi kupuuza zoezi hilo la uandikishaji kwenye daftari hilo ili kupata nafasi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Rais Samia Suluhu Hassan alijiandikisha kule Chamwino - Dodoma kwenye makazi yake na mimi nimekuja kujiandikisha kwenye makazi yangu hapa Magu.
“Napenda kutoa wito kwa wananchi kuwa wasisubiri hadi siku za mwisho ndio wajitokeze kujiandikisha badala yake wajitokeze sasa kwani zoezi halitumii muda mrefu, ndani ya dakika moja unakuwa umemaliza kujiandikisha,” amesema.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri Tax, Afisa Uchaguzi wilaya ya Magu, Mwagala Masunga amesema zoezi la kujiandikisha katika wilaya ya Magu linaendelea vizuri hasa ikizingatiwa kwa muda wa siku nne, tayari wananchi 95,157 wamejiandikisha.
Amesema zoezi hilo la kuandikisha wapiga kura uchaguzi huo lililoanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu linalenga kuandikisha wananchi 215,510.
Amesema baada ya kujiandikisha, kampeni zitaanza tarehe 20 hadi 26 Novemba mwaka huu kisha uchaguzi wenyewe tarehe 27 Novemba, 2024.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa