Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu amezungumza hayo katika siku ya kilele cha Maadhimisho ya wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu kata ya Bujora tarehe 08.03.2019. Amesema maadhimisho haya ya wanawake yalianza rasmi mwaka 1997 ambapo baada ya mwaka 2005 siku ya wanawake huadhimishwa Kitaifa kila baada ya miaka mitano.
Aidha amesema, kaulimbiu ya mwaka huu imezingatia muktadha wa vipaumbele vya nchi yetu ambapo inasema “BADILI FIKRA KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA KWA MAENDELEO ENDELEVU” . Utekelezaji wa kaulimbiu hii utawezesha wanawake katika maendeleo hivyo “tuwe na fikra chanya kuhusu nafasi ya Mwanamke, tujitafakari ni jinsi gani atashiriki katika Falsafa ya Tanzania ya Viwanda kuelekea uchumi wa kati. Serikali itaongeza fedha kwenye bajeti ya mfuko wa Wanawake ili waendelee kupata mikopo bila riba” amesema Waziri Ummy.
Amepongeza mkoa wa Mwanza kuunda kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto, aidha amezitaka Halmashauri zote nchini kuunda kamati hizo katika ngazi za wilaya, kata, vijiji na vitongiji. Pia amesema “ni wajibu kila Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kutenga asilimia 4 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kiuchumi na mikopo inayotolewa kwa wanawake lazima ihusianishwe na na kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda. Wanawake wapewe mikopo yenye tija itakayowawezesha kusonga mbele kiuchumi na sio kutoa mikopo ya laki tano”.
Wanawake wasibaki nyuma katika kuomba nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo yao, wabadili fikra na kutojiona wanyonge kifikra. Jamii itokomeze rushwa ya ngono ambapo amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kupeleka malalamiko yao TAKUKURU kama kuna viashiria vya rushwa ya ngono dhidi yao. Wakuu wa shule na Walimu Wakuu waendelee kuwasilisha taarifa ya watoto ambao wameacha shule na kuolewa kila robo kwani maboresho ya Sheria ya elimu lazima itekelezwe amesema Waziri Ummy..
Mwisho amezindua kampeni ya “Simpigi Tena” katika dhana nzima ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake. Amempongeza Shetta na kuahidi kuunga mkono juhudi zake ambapo amesihi wadau mbalimbali wajitokeze kuunga mkono Shetta katika kampeni aliyoianzisha ya “Simpigi Tena” . Aidha amemaliza kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuunga Mkono haki za Wanawake.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa