Mafunzo hayo yametolewa na watumishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoani Mwanza leo tarehe 13.07.2018 ambapo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Watumishi wa Idara mbalimbali za Halmashauri wameshiriki na kupata elimu ya mafunzo hayo. Wawezeshaji wa mafunzo hayo wamesema kuwa taratibu za kiusalama lazima zizingatiwe katika taasisi zote za Serikali kwani majanga mengi ya moto yanasababishwa na uzembe wa watu.
Aidha wamesema kuwa, miradi yote mikubwa inayotekelezwa na Halmashauri lazima ihusishe Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kuhakikisha uwepo wa usalama katika miradi hiyo. Watumishi wameshukuru kwa kupata elimu hiyo muhimu ya kujikinga na majanga ya moto na kuahidi kuwa chachu ya kuelimisha watu wengine katika maeneo wanayoishi.
Katibu Tawala Wilaya Ndugu Menruf F Nyoni amepongeza wawezeshaji hao kutoa elimu ya kuepukana na majanga hayo Katika Majengo ya Serikali na Majumbani kwani elimu hiyo itasaidia kuepukana na majanga ya moto yanayoweza kutokea kwa sababu ya uzembe. Amewaomba kuwa pindi watakapohitajika kutoa elimu tena wasisite kufika kwani ni muhimu sana na kuna taasisi nyingi za Serikali katika wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa