Na Yusuph Digossi
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Joshua Nassari , amewataka watendaji wa Kata kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa uadilifu na weledi, ili ilete tija kwa Wananchi.
DC Nassari ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi na watendaji wa kata na baadhi ya wakuu wa idara zinazohusika na kusimamia miradi ya maendeleo kilichokua na lengo la kupitia taarifa za maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeelo inayotekelezwa wilayani Magu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika leo Alhamisi Mei 30 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri DC Nassari amesema watendaji wa kata wakisimamia miradi kwa weledi na uadilifu miradi itakamilika kwa wakati na italeta tija kwa wananchi.
Aidha DC Nassari ameagiza kila mradi uwe na kamati ya kusimamia ujenzi ili kusaidia katika usimamizi wa manunuzi ya vifaa, mapokezi na utunzaji wa usalama wa vifaa.
Pia aliwaagiza watendaji wa kata kuanzia ngazi ya kata hadi vijiji kuhakikisha wanakusanya na kusimamia mapato ya kutosha ili serikali iweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amewataka watendaji wa kata kusimamia ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kuwashirikisha wananchi kikamilifu ili kusaidia kupata taarifa na kuripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa