Na Yusuph Digossi- Magu Dc
MKURUGENZI wa Elimu TAMISEMI Dkt Emmanuel Selemani Shindika ambaye anashughulikia masuala ya elimu na utawala amewaasa walimu kuacha kukopa mikopo kausha damu kwani kupitia mikopo hiyo inapelekea walimu kutofundisha kwa weledi na matokeo yake kupelekea kufeli kwa wanafunzi.
Dkt. Shindika ameyasema hayo kwenye kikao cha pamoja na walimu wa shule za Msingi na Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu kilichofanyika leo (05.06.2024) katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Magu.
Amesema baadhi ya walimu wanasalimisha hadi kadi zao za benki kwenye taasisi za fedha ili kukopa fedha zinazowalipisha riba kubwa jambo ambalo linapelekea wengi wao kua na msongo wa mawazo ambao huathiri utendaji wao wa kazi.
Alisema inafikirisha mno kuona mwalimu ana madeni mengi na makubwa kiasi hicho lakini bado serikali na jamii inamtegemea afundishe vizuri na kwa weledi ili kumpa matokeo chanya wanafunzi.
Akifikisha Salamu za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu amesema Rais anawapenda Walimu na anajua ndiyo nguzo ya Taifa hili na kwamba atawatimizia changamoto zinazo wakabili walimu ikiwa ni pamoja na kupanda vyeo,likizo,malimbikizo ya mishahara,kubadilishwa miundo pamoja na uhamisho.
Aliongeza kuwa hadi kufikia 01,Julai,2024 walimu 54 elfu watapanda vyeo kwa mserereko na Walimu 52 elfu watapanda madaraja kwa utaratibu wa kawaida na kubainisha kuwa madai na changamoto zote za walimu zitafanyiwa kazi.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Magu imekuwa ikifanya vizuri kwenye taaluma pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya sekta ya elimu.
Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Henryh Sedatale amesema Wilaya itaendelea kusimamia taaluma kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi pamoja na ujenzi wa miradi ya elimu na usimamizi wa fedha zote za sekta ya elimu wilayani magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa