Walimu wa shule za sekondari Mkoani Mwanza wametakiwa kuwasaidia wanafunzi wa kidato cha sita wanaopata ufaulu wa juu katika mitihani ya kidato cha sita inayoendeshwa na Baraza la Mitihani Tanzania ( NECTA) katika tahasusi za sayansi kupata fursa ya udadhili wa masomo unaotolewa na serikali kupitia programu ya 'Samia Scholarship' kwa lengo la kuongeza idadi ya wanasayansi nchini ambao watachangia moja kwa moja katika maendeleo.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu, Jubilate win Lawuo wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa umoja wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania Mkoa wa Mwanza ( TAHOSSA) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa CCM Wilaya ya Magu.
Akizungumza wakati wa mkutano huo DAS Lawuo amesema kumekua na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita kupata ufaulu wa juu na wana vigezo vya kupata fursa hiyo lakini hawana uelewa wa jinsi ya kuomba na kupata ufadhili wa masomo hivyo ni vyema walimu wakatumia uzoefu wao kuwasaidia wanafunzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amesema kumekuwa na matumizi makubwa ya TEHAMA katika ujifunzaji na ufundishaji hivyo ni muhimu kwa walimu kuendana na mabadiliko hayo ili kuendana na malengo ya Serikali ya kutoka elimu bora na kwenda na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia zinazoendele duniani.
Amesema Matumizi yaTEHAMA ni muhimu kwa sasa, matumizi ya karatasi na kuandika vinapotea, hivyo ni muhimu kupata ujuzi na maarifa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA katika ujifunzaji na ufundishaji .
Aidha amewataka Walimu wakuu wa shule za Sekondari Mkoa wa Mwanza kusimamia walimu kujaza taarifa katika mfumo wa Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi PEPMIS /PIPMIS na mifumo mingine inayotumiwa na watumishi na shuleni kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali hapa nchini.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa