JUMLA ya waandishi wasaidizi 43, waandishi wasaidizi wa akiba 25, waendeshaji wa vifaa vya bayometriki (BVR) 43 na waendeshaji wa vifaa bayometriki wa akiba 25 walioteuliwa kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili, wameapishwa.
Waandishi na waendesha vifaa hivyo wameapishwa leo tarehe 29 Aprili, 2025 katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Ilungu mkoani Mwanza tayari kwa kuanza zoezi hilo la uboreshaji wa daftari hilo awamu ya pili litakaloanza tarehe 1 hadi 7 Mei mwaka huu.
Akizungumza na waandishi na waendesha vifaa hivyo, Afisa Mwandikishaji Jimbo la Magu ambaye ndiye aliyewaongoza katika kiapo hicho, Mohamed Kyande amewataka waandishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia maelekezo waliyopewa.
“Tunaelewa wazi kuwa katika zoezi la awali kulikuwa na washiriki zaidi ya 580, sasa tupo washiriki 136 hivyo unapaswa kujitathmini kwa kupenya kushiriki zoezi hilo… jipongeze. Hili ni takwa la kisheria kwamba wale walioshiriki vema katika zoezi la kwanza waendelee kushiriki katika zoezi la pili.
“Katika wale 580 majina yalipelekwa na kuchujwa hivyo mkiwa hapa tunaamini mmeaminiwa hivyo nendeni mkafanye kazi ipasavyo. Lakini mjue kuwa hata huko unakokwenda unatakiwa kufanya kwa ufanisi kwa sababu utakuwa unafuatiliwa utendaji wenu. Mmepita katika tanuru la moto ni matumaini yetu kuwa hili zoezi mtalifanya vema ili zoezi linalofauata tuendelee kufanya vema,” amesema na kuongeza;
“Hiki kiapo sio suala la kawaida ni la kisheria litatumika kukuhukumu huko unakoenda, hivyo tusifanye masihara”.
Amesema zoezi halitakuwa gumu kama awali lakini pia watapewa ushirikiano kutosha ili kutekeleza majukumu yao ikiwamo kuhakikisha wanaandikisha watanzania halisi wenye sifa za kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa