Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa dini, mila na siasa katika Halmashauri ya wilaya ya Magu mkoani Mwanza wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea miradi mikubwa ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo hatua ambayo imetajwa kuwa itachochea maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Viongozi hao wametoa pongezi na shukrani hizo jana Jumatatu baada ya kutembelea miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa daraja la Sukuma, Simiyu, jengo jipya la halmashauri na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Bundlya.
Ziara hiyo maalumu iliandaliwa na Mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri, Mohamed Ramadhani.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa daraja la Sukuma lililopo kata ya Ng’haya wilayani humo, Mhandisi Hassan Habibu kutoka Tanroad Mwanza, alisema daraja hilo pamoja na barabara unganishi, linajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 11.4.
Alisema daraja hilo lenye urefu wa mita 70 na upana wa mita 11 pia litakuwa na barabara unganishi zenye urefu wa km 2.2 ambapo zitajengwa upande wa upande wa Ng’haya na Lumeji.
“Mradi ulianza mwaka jana Oktoba mwaka jana na sasa umefikia asilimia 25 kutokana na changamoto ya mvua kubwa lakini mkandarasi ataongeza speed ndani ya muda mfupi mpaka kufikia Machi mwaka 2025 atakuwa amekamilisha kazi hii,” alisema.
Akitoa pongezi hizo baada ya kutembelea daraja la Sukuma lililopo wilayani Magu, Paroko wa Parokia ya Magu Jimbo kuu la Mwanza, Padre Onesmo Shigelwa alisema madaraja katika wilaya hiyo yamekuwa changamoto kubwa katika shughuli za usafirishaji lakini ujenzi huo unaoendelea umeleta ahueni kwa wananchi.
Naye Sheikh wa wilaya ya Magu, Nuhu Zaid Khamis alisema yanayotendeka katika wilaya hiyo ni tafsiri halisi ya vitabu vya dini kwa namna serikali inavyowajali watu wake.
Mwenyekiti wa Chadema – Magu, Malimi Butage pia aliipongeza serikali kwa miradi hiyo ya maendeleo na kusisitiza kuwa miradi hiyo inaendelea kufungua shughuli za kiuchumi kwa wananchi bila kujali itikadi za kiasiasa.
Naye Mbunge wa jimbo hilo la Magu, Boniventure Kiswaga alisema akiwa kama kiunganishi kati ya Serikali na wananchi, ujenzi wa madaraja hayo ya Sukuma na Simiyu inayogharimu zaidi ya Sh biilioni 60 ni moja ya mambo aliyokuwa akiyapigia kelele bungeni kila mara.
“Kwa sababu mazao yalikuwa yanakwama kwa kukosa vivuko. Barabara hizi pia zimefikia hatua usanifu wa kujenga kwa kiwango cha lami kwenda Bariadi na Mahaha, kinachofuata ni kupata fedha. Pia ujenzi wa ‘round about’ ya kwenda Kwimba serikali imetoa bilioni 14 na mkandarasi ataanza kujenga km 10,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa jengo la utawala Kiswaga alisema hivi karibuni serikali imetoa Sh milioni 700 kumalizia ujenzi wa jengo hilo ambalo ndilo litakuwa makao makuu ya halmashauri.
Aidha, Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Mohamed Ramadhani alisema muda wowote wanaweza kuhamia kwneye jengo hilo jipya.
“Tunategemea Januari hadi Februari ndani ya jengo kutakuwa kumekamilika, na kubakia nje. Lakini pia ili kurahisishia wananchi kupata huduma hapa, halmashauri imeshatenga fedha, kwa ajili ya stendi na ninawahakikishia jengo hili litakuwa miongoni mwa majengo bora kwani hata mwananchi anayekuja kufuata huduma atapata pia huduma ya intaneti bure,” alisema.
Mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Nassari alisema ziara hiyo ililenga kuwaonesha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ili waone kwa kwa macho badala ya kuelezwa pekee.
“Tutaendelea kufanya utaratibu wa kushirikisha watu kwani maendeleo ya Magu ni ya wananchi wa Magu,” alisema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa