Halmashauri ya Wilaya ya Magu imeadhimisha siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa Desemba Mosi kila mwaka na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2024 kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Majimaji mkoani Ruvuma huku wilaya Magu ikifanyika katika viwanja vya sabasaba kata ya Magu mjini.
Lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya udhibiti UKIMWI ambayo ni ajenda ya kidunia, kutathmini muelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI nchini na kutafakari changamoto mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa Virusi vya UKIMWI(VVU).
Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika yakiwa na kauli mbiu 'Chagua njia sahihi tokomeza UKIMWI'.
Katika maadhimisho hayo huduma mbalimbali zimetolewa ikiwemo za elimu juu ya Virusi vya UKIMIWI (VVU) na matumizi sahihi ya dawa na kingatiba kwa makundi maalum bila kusahau watoto waliopo katika mazingira hatarishi ya kupata UKIMWI, upimaji wa VVU na magonjwa muambata ikiwemo magonjwa ya ngono na homa ya ini.
Akizungumza wakati akifungua maadhimisho hayo makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Marco Kabadi ameiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa