Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa John Mongela ameagiza hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya wilaya ya Magu leo tarehe 01.05.2019 katika viwanja vya Sabasaba. Amesisitiza waajiri wote wakiwemo wa makampuni binafsi kukaa na watumishi wao kwa kufuata sheria na taratibu katika suala la kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Aidha ametoa wito kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa watumishi wanapopeleka malalamiko ya stahiki zao watoe suluhisho. Maboresho yanayoendelea kufanywa katika mifuko hiyo yawe na lengo la kuwapa amani watumishi wa Umma na sio viginevyo hasa wanaostaafu baada ya kumaliza muda wao wa utumishi. “Lazima maombi ya wafanyakazi yatazingatiwa hivyo, tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kauli mbiu inayosema ‘UCHUMI WA KATI INAWEZEKENA, WAKATI WA MISHAHARA NA MASLAHI BORA KWA WAFANYAKAZI NI SASA’ ninaiunga Mkono kinachohitajika kwa wafanyakazi ni kuwa na Subira pamoja na kufanya kazi kwa mshikamano ” amesema RC Mongela.
“Katika Mkoa wa Mwanza tutahakikisha hakuna haki ya Mfanyakazi inayopotea kwani wafanyakazi wanachangia sana katika kuleta amani na utulivu katika Mkoa Wetu, kuna baadhi ya maeneo wafanyakazi wanabaguliwa ambapo sio jambo jema kufanya hivyo, katika vikao vyote vya uwakilishi lazima kuwepo na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi ili maazimio ya vikao yanapofikiwa, yawe yanafika sehemu husika nakufanyiwa kazi na kutekelezwa kwa wakati. Vyama vya wafanyakazi vipo kisheria kwa ajili ya kutatua changamoto za wafanyakazi. Tumuunge mkono Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ili tusonge mbele katika Maendeleo ya nchi yetu” amesema RC Mongela.
Awali Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Mwanza ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya wafanyakazi yanayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya, Mkuu wa mkoa wa Mwanza kuwa Mgeni Rasmi Katika Maadhimisho haya ya Kimkoa hapa Wilayani Magu na Mkuu wa Wilaya ya Magu kwa kufanya Maandalizi mazuri kwa ajili ya siku ya wafanyakazi kimkoa bila kumsahau Mkurugenzi Mtendaji (W) na timu yake. Aidha ametoa changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Mkoa wa Mwanza mbele ya Mgeni rasmi kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt Philemoni Sengati (Phd) amewataka wafanyakazi kuwa wazalendo, wafanye kazi kwa bidii na kuepuka mbinu za kizamani za kusuluhisha migogoro, bali watumie Diplomasia kudai haki. Aidha ameshukuru uongozi wa Mkoa kuleta maadhimisho haya ya wafanyakazi ya mwaka 2019 Wilayani magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa