MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Joshua Nassari amerejesha tabasamu la kijana aliyepata ulemavu wa viungo vya mguu na mkono kwa kumuwezesha kupata mguu bandia pamoja na kiti mwendo (Wheelchair).
Pia kijana huyo Ndalawa Emanuel Maduka (23) ambaye ni mkazi wa Itumbili wilayani Magu, amepatiwa fedha kiasi cha milioni tano zitakazomuwezesha kufungua biashara ya kuuza vipuri vya pikipiki katika eneo hilo.
Msaada huo umekabidhiwa leo tarehe 26 Februari, 2025 na Mkuu huyo wa wilaya mbele ya Mwenyekiti wa taasisi ya Desk and Chair Foundation – Mwanza, Alhaj Dk. Sibtain Meghjee ambao ndio walifadhili wa msaada huo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, DC Nassari aliishukuru taasisi hiyo ya Desk and Chair Foundation kwa kusaidia upatikanaji wa mguu bandia pamoja na fedha hizo za mtaji.
“Tunawashukuru sana, wamekuwa wakisaidia jamii na huyu ni mmoja wa wanufaika wa ufadhiili huu. Tulisema tusimtafutie baiskeli na mguu na kuishia hapo, kwa sababu ana ulemavu wa viungo ila sio wa akili hivyo ataendelea kutumia ile taaluma yake ya ufundi.
“Tutamfungulia biashara ya kuuza spea za pikipiki hapa Magu. Tutaifuatilia kwa karibu, hatutaki mtaji uende kupotea, tunataka tuone anatoka na kunyanyuka kwa sababu akili yake inafanya kazi,” amesema Nassari.
Aidha, Mwenyekiti wa taasisi ya Desk and Chair Foundation – Mwanza, Alhaj Dk. Sibtain Meghjee amesema baada ya kuelezwa uhitaji wa kijana huyo na Mkuu wa wilaya aliguswa na kuanza kwa kutoa kitimwendo.
“Baada ya kupata milioni 5, tulitoa hapo 700,000 ili apate mguu wa bandia. Sasa kilichobaki tumekileta ili apate mtaji. Nipongeze kwa kumpa mafunzo ya ujasiriamali namna ya kusimamia mtaji huu,” amesema.
Akishukuru kwa msaada huo, Mama kijana huyo, Gina Efugomo alisema ataenda kumpa ushirikiano wa kutosha mwanaye huyo ili aweze kusimamia vema mtaji aliopewa.
Naye Ndalawa ambaye alipata ulemavu huo mwaka jana wakati akiwa kwenye majukumu yake ya ufundi wa umeme wa magari, mbali na kumshukuru mkuu wa wilaya pamoja na taasisi hiyo amesema sasa kwa mtaji huo anakwenda kuinuka tena.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa