Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Joseph G. Kakunda (Mb) amefanya ziara Wilayani Magu na kuweka jiwe la msingi katika shule mpya ya Sekondari Lumve iliyopo kata ya Bujora tarehe 16.03.2018. Amepongeza Jitihada na ushirikiano unaoonyeshwa baina ya Viongozi na wananchi katika kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari Lumve.
Amesisitiza kuendelea kushirikisha wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo kwani Serikali haijakataza wananchi kuchangia maendeleo, bali michango yote inayohusiana na maendeleo inatakiwa iratibiwe na Serikali ya Kijiji husika na kupitisha kiwango cha kuchangia kulingana na kaya zilizopo kwa kufuata taratibu zilizopo na sio kuadhibu wanafunzi.
Amesema kuwa, kuna mambo mengi yanayohitajika ili shule ya sekondari Lumve itimize vigezo vya kusajiriwa hivyo viongozi wahakikishe wanasimamia ili majengo mengine kama vile maabara na jengo la utawala yakamilike kwa wakati.
Pia ameshauri viongozi wa vyama vingine vya siasa waunge mkono miradi ya maendeleo katika maeneo yao kwani huu ndio mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano kuwaletea wananchi wake maendeleo. “Serikali imeleta Tshs. 60,000,000.00 ya ujenzi wa Maabara kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Bujora” Amepongeza Diwani wa kata ya Bujora kwa kuchangia Tshs. 9,000,000.00 katika ujenzi wa shule ya sekondari Lumve.
Naibu Waziri OR TAMISEMI amepongeza usimamizi mzuri unaofanyika kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Itumbili pamoja na kuwa shule hiyo maalumu ina changamoto mbalimbali zinazoikabili. Amesisitiza shule hiyo ipewe kipaumbele na kuona utaratibu wa kuongeza shule nyingine zenye mahitaji maalum katika wilaya ya Magu.
Aidha amezungumza na watumishi ambapo amewasisitiza kufanya kazi kwa weledi kwani Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha huduma kwa wananchi wake katika sekta za elimu, afya na Maji. “Tumuunge Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwani ana Uthubutu wa hali ya Juu katika kufanya Maamuzi na kutumia Rasilimali za ndani katika kutekeleza miradi mikubwa”. Ushirikiano uliopo uendelezwe kwani kwa kufanya hivyo wananchi watapata maendeleo.
Mhe.Naibu waziri OR TAMISEMI Akiweka Jiwe la Msingi katika Shule ya Sekondari Lumve
Mhe. Naibu waziri OR TAMISEMI Akisikiliza Taarifa ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lumve
Mhe. Naibu Waziri OR TAMISEMI Akisikiliza Taarifa ya uendeshaji wa Shule ya Watoto wenye Mahitaji Maalum Itumbili
Mhe. Naibu Waziri OR TAMISEMI Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa