Naibu katibu mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Gerald Mweli anaeshughulikia elimu ameyasema hayo wakati alipotembelea Halmashauri ya Magu leo tarehe 11.03.2020. akiwa katika ziara amezungumza na uongozi wa wilaya, Maafisaelimu Kata, wakuu wa shule, walimu wakuu pamoja na baadhi ya walimu wa shule za sekondari na msingi katika ukumbi wa shule ya Sekondari Magu.
Amesema “Mahusiano yaliyopo kati ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji (W) na watumishi wengine ni mazuri kwani wanafanya kazi kwa pamoja”. Kuhusu changamoto za Madaraja na madai mbalimbali kwa watumishi wa umma amesema Serikali inayafanyia kazi ili kila mtumishi alipwe stahili zake.
Amesisitiza kusimamia elimu kwani kipaumbele ni taaluma inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu katika Taifa letu. “Serikali ya awamu ya tano inafanya jitihada kubwa katika suala la kuboresha elimu kwa kujenga miundombinu mbalimbali na zaidi ya shule 250 mpya zimejengwa nchini hivyo viongozi simamieni elimu, taaluma na watumishi waliopo chini yenu na msisite kuchukua maamuzi. Katika suala la changamoto ya upungufu wa walimu wa Masomo ya sayansi na Hisabati endeleeni kutumia walimu waliopo vizuri wakati serikali inajipanga kuajiri walimu wapya” amesema Naibu katibu Mkuu.
Mkurugenzi wa Elimu OR-TAMISEMI Bw Julius Nestory ametoa mwelekeo wa elimu inayopaswa katika kuleta mapinduzi makubwa ambapo amesisitiza sana suala la taaluma, kutumia fedha za miundombinu kwa kuzingatia utaratibu, na maadili kuhusiana na nidhamu za walimu na wanafunzi. “Wakuu wa shule wafuatilie masomo yanayofundishwa darasani na wasimamie walimu kufundisha mada zote kwa muda na kwa kina”.
Amesema “Msimamizi wa elimu wa awamu ya tano anapaswa kuwasikiliza watu, kufanya maamuzi, kuwa na siri, kuwa na maadili, kufanya kazi zinye matokeo na kuwa mbunifu”. “Maelekezo ya Serikali ni kwamba Maafisaelimu Kata wakae katika vituo vyao vya kazi, kila mkuu wa shule / mwalimu mkuu kufundisha angalau vipindi 4 kwa wiki, maafisaelimu kata na wakuu wa shule angalau wawe na shahada na kukata mshahara kwa walimu wasiotimiza wajibu wao kwa kutofundisha vipindi vyote” amesema Mkurugenzi wa Elimu OR-TAMISEMI.
Mkuu wa wilaya ya Magu Dr. Philemon Sengati (PhD) ametoa pongezi kwa Naibu katibu mkuu na timu yake kwa kazi anazozifanya za kupunguza changamoto zinazowakabili watumishi. “ watumishi wa wilaya ya Magu ni wachapakazi sana na kwa pamoja tumeanzisha mfuko wa elimu ambapo watumishi wote ni wadau” . amemuomba Naibu katibu mkuu kuchukua changamoto za watumishi hasa madeni na madaraja sambamba na ombi la uanzishaji wa shule za kidato cha tano na sita (A-Level) angalau kila tarafa iwe na shule moja ya aina hiyo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji (W) Bw. Lutengano G. Mwalwiba amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa mishahara ya watumishi kwa wakati na ametaja mafanikio yaliyotokana na fedha za EP4R tangu mwaka 2016 hadi 2019 katika wilaya ya Magu zilizotumika katika ujenzi wa miundombu mbalimbali ya shule kama vile madarasa 52, mabweni 4 maktaba 1 na matundu ya vyoo vya wanafuzi, utengenezaji wa madawati na kurekebisha ikama ya walimu. Aidha ameomba madai wa walimu yaliyohakikiwa na kukubalika yafikiriwe ili walimu walipwe kwani ni madeni ya muda mrefu.
Aidha amemuomba Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Kukabidhi vyeti vya pongezi kwa Mkuu wa wilaya ya Magu, Mbunge Jimbo la Magu, na Idara ya elimu Msingi kwa kutambua jitihada zao katika kuletea Magu Maendeleo. Vile vile amemuomba kukabidhi mfano wa hundi yenye Jumla ya Tshs. 116,012,255.00 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama asilimia 10 inayorudi kwa wananchi kama mkopo bila riba na Naibu waziri amefanya hivyo.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Akimpatia DC Magu Cheti cha Pongezi kwa jitihada anazofanya katika kuiletea Magu maendeleo
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI akimpatia Afisaelimu Msingi Cheti cha pongezi kwa kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba 2019
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI akikabidhi Mfano wa Hundi yenye Tshs.116,012,255.00 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa