Mwenge huo wa Uhuru, umepokelewa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Tarehe 19.08.2017. Ukiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Magu umeweza kuzidua na Kuweka mawe ya Msingi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2017 unasema “Shiriki kukuza uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu” . (Mapambano dhidi ya dawa za kulevya tuwajali na tuwasikilize watoto na vijana, Tuungane kwa pamoja kupambana dhidi ya Rushwa kwa maendeleo, amani na usalama wa taifa letu, Tanzania bila Maambukizi mapya unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI Inawezekana ifikapo Mwaka 2030, Shiriki Kutokomeza malaria kabisa kwa Manufaa ya Jamii).
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Amour Hamad Amour amepongeza Halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kutekeleza Miradi ya Maendeleo kwa kiwango na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Viongozi wote. Amesema kuwepo na jitihada za kuanzisha Viwanda kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na Teknolojia. Viongozi waone umuhimu wa kuanzisha Viwanda katika wilaya ya Magu na kujali bidhaa zinazozalishwa ndani ya Wilaya. Wanaoendesha viwanda wafuate taratibu na sheria za Serikali ili kuwezesha mapato kupatikana kwa kutoa kodi ya Huduma. Aidha amesisitiza wananchi kuibua na kuanzisha miradi wenyewe kwani kwa kufanya hivyo Serikali itaongeza nguvu kwenye miradi hiyo kama sera inavyoelekeza.
Pia amesema wana Magu wadumishe mapambano dhidi ya Rushwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo, tupige vita Maambukizi mapya ya UKIMWI na Unyanyapaa kwa WAVIU. Vijana watumie nguvu zao kuwekeza katika viwanda na sio kutumia madawa ya kulevya. Halmashauri itenge fedha Asilimia 10 kwa ajili ya kukopesha Vijana na Wanawake kwa maendeleo yao. Aidha amesema miradi iliyotembelewa yote ina tija katika kuhakikisha maendeleo endelevu. Amemaliza kwa kushauri wananchi kuwa, mazao yanayolimwa yasiuzwe nje ya nchi bali yatumike kama mali ghafi katika viwanda vyetu na kuongeza thamani kwani kwa kufaya hivyo tunaunga mkono juhudi anazofanya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli za kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa