Mkuu wa Wilaya ya Magu Mheshimiwa Khadija Nyembo amekagua shughuli mbalimbali za ujasiriamali zinazofanywa na wanawake katika Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 08.03.2018 katika Kata ya Kandawe. Ameahidi kushughulikia changamoto kama zilivyoainishwa katika risala ambapo wilaya itaimarisha masuala yafuatayo kwa lengo la kuziondoa changamoto hizo;-
Kuendeleza teknolojia ya uhakika wa chakula na lishe.
Kuimarisha program za mafunzo ya lishe bora kwa wanawake, watoto na jamii kama njia ya kinga ya magonjwa nyemelezi.
Kuongeza uelewa kwa wanawake juu ya masuala ya Jinsia
Kuhakikisha kila familia inahifadhi chakula cha kutosha kwa matumizi na ziada.
Kuimarisha huduma za afya na uzazi salama na kuhamasisha wanawake kupima afya zao na kujiunga kwenye mfuko wa afya ya jamii (CHF).
Kuhakikisha wanawake wanashirikishwa katika uongozi wa ngazi zote.
Kuhakikisha Halmashauri yetu inachangia kikamilifu katika mfuko wa maendeleo ya Wanawake na Vijana.
Kuanzisha mtaa wa viwanda vidogo vidogo kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) Mwanza.
Ameendelea kwa kueleza kwamba, Mkakati wa elimu ambao Wilaya imejiwekea ni katika kufanya jitihada za kuondoa hali ya ubaguzi wa aina zote katika jamii, sera ya elimu inahakikisha kuwa, wasichana wanapata nafasi sawa ya kuingia katika mfumo rasmi wa elimu, pia kuwawezesha kuzitumia nafasi hizo kwa ukamilifu zaidi.
Aidha amesema Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanafanyika kila mwaka kwa kuambatana na kauli mbiu ambayo hutoa mkazo kuhusu jambo fulani. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI”. “Lengo la kauli mbiu hii ni kuifanya jamii itambue kuwa msingi wa maendeleo katika jamii unachochewa na ushiriki wa mwanamke katika uchumi kwa njia ya viwanda unaoambatana na usawa wa jinsia. Ni jambo la muhimu sana katika kumwendeleza mwanamke na kuondoa unyanyasaji, hivyo tunatakiwa kuendeleza mapambano kwa kasi zaidi na kuzidi kuhamasisha jamii ili kuamsha ari hasa wanaume waendelee kutambua kuwa wanawake ni washirika wakubwa katika suala zima la maendeleo, hivyo kwa pamoja tunaweza kujenga nchi yetu”.
Amemaliza kwa kusema kwamba, Maendeleo ndani ya wilaya yetu yanaletwa kwa ushirikiano kati ya wanawake, wanaume, serikali na wadau mbalimbali. “Nimefurahishwa sana kwa kushiriki kwenu kikamilifu, nina kila sababu ya kushukuru kwa ushirikiano wenu”.
Mkuu wa Wilaya ya Magu akipanda mti katika Maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani (chanzo: siku ya wanawake)
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa