Mkutano wa Kawaida baraza la madiwani umefanyika tarehe 05.05.2017 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu kwa ajili ya kupitia taarifa mbalimbali za utekelezaji kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2016/2017 (Januari-Machi, 2017).
Katika Mkutano huo Bi. C. Bigambo amepongeza Halmashauri ya magu kupata hati safi, ameshauri wataalam wa halmashauri kusaidia Wahe. Madiwani kufanya maamuzi sahihi. Aidha amesisitiza Halmashauri ifanye juhudi za kukusanya mapato ya ndani kwani lengo lililopo ni kufikia asilimia 100 kwa kila Halmashauri.
Dr. Subi (RMO) amepongeza Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia vizuri majukumu yao pamoja na kudai takwimu mbalimbali kutoka kwa wataalam. Ameshauri Halmashauri kupitisha kiwango cha Tshs. 10,000/= kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwani kiwango kilichopo kwa sasa Tshs. 5000 ni kidogo, kwa kufanya hivyo huduma za afya zitaendelea kuboreshwa katika maeneo yote. Katika vituo vya Afya kwa sasa kuna dawa muhimu zaidi ya asilimia 80 na Serikali inaendelea kufanya jitihada kwenye suala zima la ununuzi wa dawa ikiwemo ni pamoja na kutenga fedha nyingi za kununua Madawa. Aidha ameshauri Madiwani kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwenye vituo vya Afya na zahanati kuona huduma zinazotolewa kwa wananchi na kusimamia uboreshaji wa miundombinu mbalimbali. Amesema kuwa Wakurugenzi wameagizwa kila robo wafanye ukaguzi wa dawa jinsi zinavyotolewa na zinavyotumika kwenye vituo vyote vya afya.
Akichangia hoja Mheshimiwa Destery Kiswaga Mbunge Jimbo la Magu, ameshauri wenyeviti wa WDC kuhamasisha wananchi ili wajenge zahanati kwenye maeneo yao kwani vijiji 40 kati ya 82 havina huduma za Afya. Pia wananchi wahamasishwe kuchangia Tshs. 10,000 za CHF ili kuweza kuendana na kasi ya maendeleo badala ya kuchangia Tshs. 5000 ambayo haitoshi. Ameeleza kuwa kipaumbele cha mfuko wa jimbo ni ujenzi wa zahanati ambapo ameomba Wahe. Madiwani kusaidia kuhamashisha wananchi.
Mhe. Hilali Elisha (Mwenyekiti wa Halmashauri) ameshauri kamati ya Elimu Afya na Maji kuchakata suala la kupandisha tozo ya CHF kutoka Tshs 5000 hadi 10,000 ili mwaka wa fedha 2017/18 Halmashauri ianze kutoza Tshs 10,000/=, kwa kufanya hivyo wananchi watapata huduma bora. aidha amesisitiza wajumbe kusimamia miradi ya maendeleo kwenye kata zao kwa kushurikiana na wataalam.
Mkurugenzi Mtendaji (W) amepongeza mbunge wa jimbo la Magu kwa kazi nzuri anayofanya ya kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Magu kwani anachangia Halmashauri kupata fedha za Miradi ya maendeleo. Ameshauri wajumbe kuwa fedha zinapokuwa zinapelekwa kwenye kata zitumike kwa miradi iliyokusudiwa kuliko kubaki kwenye akaunti za kata.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa