Wilaya ya Magu imekusudia kuendelea kupambana na umaskini na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wake kwa kutoa huduma bora zenye kulenga mahitaji yao kuwashirikisha kwenye mpango ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Desemba 09, 2023 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo wakati wa kongamano la kuadhimisha miaka 62 ya uhuru liliofanyika katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Magu.
Akihutubia wakati wa kongamano hilo katibu Tawala Lawuo amesema kupitia maadhimisho hayo wananchi wanasisitizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi kwani maendeleo ya Wilaya yanaletwa na wananchi wenyewe.
"Wana Magu napenda kuwakumbusha kwamba, Serikali, wananchi na wadau mbalimbali tushirikiane kwa pamoja na tunaweza kufikia uchumi wa juu" amesema
Ameongeza kuwa ukatili wa aina zote kwa wananchi umepungua kwani Serikali imejielekeza kutoa elimu kwa makundi mbalimbali juu ya faida na hasara za ukatili wa aina zote kwa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Fidelica G. Myovella amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha za maendeleo Wilayani Magu na Taifa zima kwani wananchi wanaona miradi mingi ikiendelea hapa nchini.
Akitaja mafanikio yaliyopatikana Wilayani humo tangu nchi ipate uhuru ni pamoja na Kuongezeka kwa miundombinu ya barabara katika Wilaya na Taifa kwa ujumla, Ujenzi wa Shule za Sekondari na Msingi umeongezeka, Upatikanaji wa maji safi na salama na kukua kwa uchumi na maendeleo ya Wilaya.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa