HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu inatarajia kutumia Sh milioni 92 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati 1300 ambayo yanatarajiwa kusambazwa kwa shule za sekondari na msingi zenye uhaba wa samani hizo pamoja na shule mpya ambazo zinaendelea kufunguliwa wilayani humo.
Hayo yameelezwa jana tarehe 20 Mei, 2025 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simon Mpandalume wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Sayaka, Kisamba na Nsola.
Mpandalume ambaye alifanya ziara katika vijiji hivyo vilivyoko kata ya Lububu, amewahakikishia wananchi hao kuwa Shule ya Sekondari Sayaka inatarajiwa kufunguliwa miezi michache ijayo pindi wanafunzi watakaporejea kutoka kwenye likizo.
“Tayari halmashauri imekabidhi mkandarasi kazi hii ya kutengeneza madawati na katika shule hii ya Sayaka, tutapata madawati 200,” amesema.
Pia amesisitiza shule ya msingi Nyashimba nayo pia itaanza kufunguliwa wiki ijayo huku jitihada hizo zikiwa na lengo la kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kupata elimu.
“Baada ya shule ya sekondari Sayaka kufunguliwa, tutaipandisha hadhi shule ya sekondari Lububu iweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwani mrundikano wa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa,” amesema na kusisitiza tayari halmashauri imeandika barua kwenda Serikali kuu kupandisha hadhi shule tatu za sekondari ikiwamo Lububu.
Pamoja na mambo mengine, amewahakikishia wananchi wa Nsola na Kisamba kuwa, ujenzi wa zahati za vijiji hivyo utaendelea kwani halmashauri tayari imetenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa