Kituo cha afya Kahangara kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, kimeshika nafasi ya tatu kitaifa katika utoaji wa huduma bora za afya na kikiwa kinara katika Mkoa wa Mwanza. Kituo hicho kilikarabatiwa mwaka 2017, na kukaguliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa hapo Februari 18, 2018.
Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Magu, Lutengano Mwalwiba amepongeza ari ya watumishi wa kada ya afya na mtazamo wao chanya katika utoaji wa huduma katika vituo vya afya na zahanati, aidha amesema kuwa mwaka, 2018, “tumeshika nafasi ya tatu kitaifa tukitanguliwa na vituo vya Katavi na Sirari, Lakini pia kituo hiki kimezungukwa na zahanati za Bugabu, John Mongela, Mwamanga, Kinango na Ijinga hivyo kinahudumia takribani wakazi 20,540. Wito wangu kwa watumishi wote ni kwamba, wajitume kazini bila kulazimishwa na haya ndiyo matokeo chanya kama yaliyopatikana Kahangara ni juhudi za makusudi”.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu Dr.Maduhu Nindwa amefafanua vigezo ambavyo hutumiwa na wizara ya afya katika kupima utoaji wahuduma bora, baadhi ya vigezo ni Ubora wa miundombinu iliyojengwa inayopelekea upatikanaji wa huduma bora, Vifaa tiba,uendeshaji wa ukarabati kituo uliofanyika kwa ubora na viwango vinavyokidhi, Kuwahi kuyatumia majengo baada ya ukarabati kwa wakati, Ushirikiano wa watumishi wote wa kituo cha afya kahangara na ari yao ya utoaji huduma kwa kufuata maadili na kuwajali wateja kwa mujibu wa kanuni za kitabibu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa