Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari ameagiza watendaji wa kata kuongeza ubunifu wa kuwashawishi akina mama wajawazito kuzingatia ulaji bora unaojumuisha matunda na mboga za majani vilevile kutumia vidonge vya kuongeza damu ili kuondokana na udumavu kwa watoto na vifo vinavyozuilika kwa akina mama wakati wa kujifungua.
Mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari (katikati) akiongoza kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhan na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Jubilate Lawuo.
Pia amewataka watendaji wa kata na vijiji kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya kijiji kwa ajili ya kutoa elimu ya shughuli za lishe kwa wananchi katika Halmashauri ya Magu mkoani Mwanza.
Nassari ametoa maagizo hayo leo Ijumaa tarehe 28 Machi, 2025 katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Lishe kipindi cha robo ya pili Oktoba- Disemba 2024/2025.
Amewataka wajumbe na wakuu wa idara kuendelea na ufuatiliaji na usimamizi wa hali ya lishe katika maeneo yao na kupanda miti ya matunda na mbogamboga kama moja ya njia ya kuhamasisha jamii kuzingatia mlo bora.
"Lakini pia natoa wito mtumie majukwaa mbalimbali ikiwamo ya kidini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi katika utoaji wa elimu hii ya lishe," amesema.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani ambaye ni katibu wa kamati, amesema tayari halmashauri hiyo imeshaanza kupanda miti ya matunda katika shule mbalimbali ikiwa ni moja ya njia ya kuhamasisha ulaji wa matunda yatakayowasaidia watoto kuondokana na udumavu.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Magdalena Lema wakati akiwasilisha taarifa ya viashiria vya utekelezaji wa Maendeleo ya shughuli za Lishe Wilayani Magu na kadi alama, ameeleza kwamba hali ya utoaji wa Lishe katika shule za msingi na Sekondari imeendelea kuimarika kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2024/2025 inayoishia Disemba 2025 na watoto wanaendelea kupata mlo mmoja wakati wa masomo na wazazi na wananchi wamehamasika katika suala la uchangiaji wa chakula mashuleni.
Aidha, amewakumbusha Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri kufuatilia na kusimamia utekelezaji pamoja na kuhakikisha wanafanya Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ambayo kwa mujibu wa taratibu na sharia hufanyika mara moja kwa kila robo ya mwaka kwa lengo la kutoa elimu na hamasa ya shughuli za Lishe kwa Wananchi ili kuweza kufikia malengo ya mkataba wa lishe.
Katika kikao hicho cha Kamati ya Lishe ngazi ya Halmashauri kimewashirikisha Wakuu wa Idara na Wataalam mbalimbali kutoka sekta za afya, elimu, kilimo, na maendeleo ya jamii, pamoja na viongozi wa dini ambao wameahidi kutumia majukwaa yao kuhamasisha mbinu za kupata mlo bora.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa