WAKATI shamrashamra za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani zikiendelea kushika kasi, wanawake katika wilaya ya Magu wameaswa kutambua haki zao na kuzingatia malezi yenye maadili kwa watoto ili kuzalisha kizazi kitakachokuwa na tija kwa Taifa.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano tarehe 5 Machi, 2025 na Afisa Tarafa ya Itumbili, Emanuel Mbila kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari katika maadhimisho ya siku ya wanawake ki-wilaya yaliyofanyika Magu Mjini.
Mbila amewatahadharisha wanawake kuzingatia malengo ya kauli mbiu ya siku hiyo ya wanawake inayowataka kutambua haki zao pindi wanapotendewa ukatili wa kijinsia au kunyanyaswa kujua njia sahihi za kupata haki zao.
Pia Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika wilaya ya Magu, Susan Mwendi naye amewaasa wanawake kuzingatia malezi yenye maadili kwa watoto wao hasa katika kipindi hiki ambacho dunia imevamiwa na tabia hatarishi ikiwa ukatili wa kijinsia na kingono ikiwamo vitendo vya ushoga na ulawiti.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wilaya ya Magu, Amina Rashid amesema ukatili wa kingono umeendelea kuwa changamoto kubwa katika wilaya hiyo hivyo ni vema kukafanyika jitihada za haraka katika kudhibiti matukio hayo ambayo kwa mwaka jana pekee matukio 688 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa