Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu leo Alhamisi imekutana kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe katika kipindi cha robo ya pili Oktoba hadi Disemba mwaka 2024/2025.
Katika kikao hicho kilichofanyika wilayani Magu mkoani Mwanza na kuongozwa na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Benjamini Mwailagila, wajumbe wameeleza kuridhishwa na taarifa za utekelezaji wa shughuli hizo.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Lishe Wilaya ya Magu, Magdalena Lema, mojawapo ya shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kutoa elimu ya lishe na kufanya tathmini ya lishe katika kaya zenye watoto chini ya miaka mitano, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kwa kupitia wahudumu ngazi ya jamii.
“Jumla ya wazazi/ walezi 77,482 wa watoto chini ya miaka mitano walipata elimu ya ulishaji sawa na asilimia 90.9.
“Pia jumla ya akina mama 33,400 wajawazito, wanaonyonyesha na walezi wa watoto chini ya miaka mitano, walipata elimu ya lishe na ulaji bora unaofaa kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula pindi wanapofika kliniki kujua maendeleo ya mtoto,” amesema.
Poa amesema wamefanikiwa kutoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto 16 waliokuwa na utapiamlo mkali na kupona kabisa.
Aidha, kwa upande wake Mwailagila ameagiza kamati hiyo kuhakikisha watendaji wote wa kata kuendelea kusimamiwa kwa karibu ili kuisaidia serikali kutekeleza malengo yaliyokusudiwa katika upande wa lishe.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa