Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiongozwa na Mwenyekiti Bw. Mpandalume Simon imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Katika ziara hiyo kamati ilitembelea mradi wa maji Magu Mjini kwenda Nyan'gahanga- Iseni ambao ulianza kutekelezwa rasmi Februari 18, 2022 na unategemea kukamilika Mwezi Disemba 2023 ambapo ukikamilika utahudumia wananchi wapatao 31,090 kutoka kwenye vijiji vitano ambavyo ni Mwamibanga , Buhumbi, Nyashoni , Nyan'gahanga na Iseni.
Pia kamati hiyo ilitembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa mradi wa maji Magu Mjini Kwenda Sagani- Mwamabanza ambao umefikia asilimia 70 na ulianza kutekelezwa Mwezi Machi 2022 kwa kutumia Mkandarasi M\S. Chabhoke Costruction Co. LTD kupitia fedha za Programu ya Lipa kwa matokeo ( PforR) , mradi huu ukikamiliika unategemea kuhudumia vijiji vya Sagani, Salongw'e, Mwalinha, Mwamabanza na Mwateleshi, ambapo wananchi wapatao 23,953 watanufaika na huduma ya maji.
Mradi mwingine uliotembelewa na kamati hiyo ni Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Kahangara ambao ulianza kutoa huduma ya maji kwa jamii mwaka 1981 ambapo kwa muda huo wote ulikuwa na mtandao wa mabomba yenye urefu wa 2.4 km na ulikua unatumia chanzo cha kisima kilichofungwa pampu kufikisha maji kwenye tanki la ukubwa wa lita 42,000 na ukiwa unahudumia watu 2,456 kabla ya ukarabati mwaka 2019.
Vilevile Kamati ya Fedha ilitembelea chanzo cha mradi wa maji Magu mjini kwenda Mwamabanza ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria ambao unapatikana katika Kijiji cha Bugabu Kata ya Kahangara Wilayani Magu.
Katika Ziara hiyo Kamati ya Fedha iliambatana na Wataalamu kutoka Wakala wa Maji Vijijini RUWASA Wilaya ya Magu na baadhi ya Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa