Pongezi hizo zimetolewa katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani Uliofanyika tarehe 15.05.2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Akitoa pongezi hizo AAS Bi. Christina Bigambo amesema Halmashauri iendelee kusimamia ubora wa miradi ya maendeleo, kutunza kumbukumbu zinazohitajika katika ukaguzi na kujibu hoja za ukaguzi kwa wakati na kuepuka hoja mpya kwani kufanya hivyo Halmashauri itaendelea kupata hati safi.
Katika suala la kuanzisha kidato cha tano na Sita na ujenzi wa shule mpya za Sekondari wajumbe wa Baraza hilo wameridhia kuanzisha Ujenzi wa Madarasa ya Kidato cha Tano na sita katika shule ya Sekondari Kinango. Baada ya Wajumbe Kuridhia ombi hilo Bi Christina Bigambo ameshauri Halmashauri kuepuka kulipa Fidia katika maeneo yanayotarajiwa kujengwa shule mpya za Sekondari na kuepuka migogoro ya ardhi. Pia amesema Halmashauri iangalie namna ya kutoa asilimia 10 za wanawake na vijana kwani ni agizo la Serikali.
Kuhusu Kikosi Kazi cha kudhibiti Uvuvi haramu katika ziwa Victoria, wajumbe wa Baraza hilo wameshauri Serikali kutoa elimu kuhusiana na uvuvi haramu na madhara yake ili waache kutumia nyavu haramu ambazo hazihitajiki kuliko kutoza faini kubwa ambayo haiwasaidii wananchi kwani wengi wao hawana elimu.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Magu ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama amesema wananchi waelimishwe kuacha kutunza nyavu haramu majumbani badala yake waziteketeze. Pia amesema “Halmashauri ya Magu Itanunua Pamba mwaka huu Kupitia AMCOS na wananchi wasikopwe pindi ununuzi wa zao hilo utakapoanza”.
Mheshimiwa Hilali Elisha ambae pia Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani amemaliza kwa kusisitiza Wajumbe wa Baraza hilo kuhamasisha wananchi kuanzisha miradi ya Maendeleo kwani Halmashauri itapeleka fedha kwenye miradi iliyoanzishwa na wananchi katika maeneo husika.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa