KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Kyande amewataka maofisa ugani wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanatumia kwa malengo yaliyokusudiwa pikipiki walizogawiwa na Serikali kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
Kyande ametoa maagizo hayo leo tarehe 14 Januari 2025 wakati akiwagawia namba za usajili ‘plate number’ maofisa hao mjini Magu mkoani Mwanza.
Amesema lengo la kuwagawia namba hizo za usajili ni kuhakikisha pikipiki hizo 33 zinatumika kwa usahihi ili kuondoa minong’ono inayodaiwa kuzuka kuhusu matumizi yanayokiuka maadili ya umma.
“Ndugu zangu Serikali inatujali, kwa sababu mimi nimefanya kazi kwenye sekta hii ya kilimo kwa zaidi ya miaka 30 sasa lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwajali zaidi na kuwagawia pikipiki hizi, hivyo naomba muende mkazitumie kutoa huduma stahiki kwa wananchi,” amesema Kyande.
Aidha, mmoja wa maofisa ugani hao, Zawadi Madoshi alimshukuru mkurugenzi huyo kwa kuwapatia namba hizo za usajili hasa ikizingatiwa awali walivyogawiwa pikipiki hizo walikuwa wanazitumia bila utambulisho wowote jambo ambalo liliwafanya kutafsiriwa vibaya kwa jamii.
“Hakika sasa tukiwa kwenye kituo chetu cha kazi, namba hizi za usajili zinatutambulisha kama ofisa wa serikali na kuturahisishia majukumu yetu ya kila siku,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa