Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh Joshua Nassari ameongoza kikao cha thamhini ya mkataba wa lishe Wilaya ya Magu kipindi cha robo ya tatu Januari- Machi 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho DC Nassari amesisitiza suala la utoaji wa chakula kwa shule zote kwa asilimia 100 na wanafunzi wote wapate chakula lengo ikiwa ni kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao pia kupambana na athari za lishe duni ikiwemo udumavu.
Aidha amewataka watendaji wa kata kusimamia kuhakikisha kila kaya inakua na choo bora na kuzingatia suala la usafi ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kua jamii yenye lishe bora.
Vilevile DC Nassari amewaelekeza watendaji kuwasilisha sheria ndogo ndogo za utekelezaji wa afua za lishe katika maeneo yao ili kurahisisha utekelezaji wa viashiria vyote 11 vinavyopimwa katika utoaji wa huduma za lishe vitekelezwe vizuri kwa kufikia hali nzuri ya utekelezaji wa mkataba wa lishe.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amewataka wajumbe wa kikao hicho kufahamu kuwa lishe ndio msingi wa kila kitu hivyo kikao hicho ni muhimu katika uboreshaji wa lishe katika jamii na kuwasihi kusimamia afua za lishe kwenye maeneo yao kwa kuzingatia vigezo vya Kitaifa ili kuwa na Jamii yenye afya bora.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa