Mkuu wa Wilaya ya Magu Dr. Philemon Sengati amezindua Kampeni ya kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto, uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo kata ya Magu Mjini leo tarehe 30.09.2019. Amesema kuwa, Msingi wa kampeni hizi zinazo zinduliwa leo zinatokana na kuwepo kwa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA-2017/18-2021/22) ambao ni mpango kazi wa miaka mitano ulio andaliwa na serikali lengo kuu likiwa ni kutokomeza au kumaliza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika nchi yetu ya Tanzania.
“Jamii zetu lazima zitambue kuwa Wilaya yetu ya Magu haipo salama kwa kuwa matendo ya ukatili yapo na yanatokea kila siku. Ni jukumu la kila mmoja sasa kuchukua hatua za kukomesha kabisa vitendo vya ukatili vinavyofanywa kwa wanawake na watoto” amesema Dr. Sengati.
Ameendelea kusema kwamba, Halmashauri ya wilaya ya Magu itaendelea kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto ikiwa ni pamoja kuelimisha jamii kuwajibika ipasavyo katika kuwasaidia na kuwahudumia waathirika wa ukatili. “Pia niwaombe viongozi ngazi zote kwa kushirikiana na Halmashauri kutoa taarifa na kuchukua hatua za haraka pale haki za wanawake na watoto zinapokiukwa pamoja na haki za watu wengine katika jamii”.
“Niwaombe wananchi wote kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, viongozi wa madhehebu ya dini, viongozi wa vyama vya siasa na kila mtu kwa nafasi yake tuendelee kulaani na kukumea kwa nguvu zetu zote vitendo vyote vya ukatili vinavyotokea katika maeneo yetu” amesema Dr Sengati.
Aidha DC ametoa shukurani kwa shirika la KIVULINI ambalo limekuwa mstari wambele kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali kuhakikisha jamii yetu ya Magu na Tanzania kwa ujumla inakuwa salama na jamii inaishi kwa amani na upendo na ikiondokana na vitendo vya ukatili vinavyorudisha nyuma maendeleo na kuwanyima watu haki zao za msingi zikiwemo haki ya kuishi, kupata elimu, haki ya kusikilizwa, haki ya kuthaminiwa na nyingine nyingi.
“Lakini nitumie fursa hii kuwashukuru walioandaa uzinduzi huu ikiwa ni pamoja na uongozi wa kata zote tatu za hapa mjini ambazo ni Magu mjini, Isandula na Itumbili. Sambamba na hilo niipongeze Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya kwa kuratibu shughuli hii muhimu kupitia kwa maafisa walio chini yake ambao ni kitengo cha ustawi wa jamii, Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Idara ya maendeleo ya Jamii, Idara ya Afya nanyi nginezo. Hongereni sana, kazi yenu ni njema. Aidha nawapongeza wadau wengine wote walioshiriki likiwemo Jeshi la polisi, mahakama ya Wilaya kufanikisha shughuli hii muhimu. Kwa namna ya pekee niwashukuru wananchi wote waliotoka sehemu mbalimbali za wilaya yetu kuja kushiriki katika siku hii maalumu.
“Magu ni Kusema na Kutenda, Kazi kwa Maendeleo”
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa