Mkuu wa Wilaya Magu Dkt. Philemon Sengati amekabidhi fedha kiasi cha Tshs 2,000,000.00 kwa Mwalimu mkuu wa Shule msingi Nyalikungu ambazo zimetolewa na aliyewahi kuwa mwanafunzi wa shule hiyo zaidi ya miaka 30 iliyopita Dr. Stergomena Tax ambaye sasa hivi ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC).
Dr, Tax ametembelea shule hiyo aliyosoma mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa katika mapumziko ya mwisho wa mwaka nyumbani kwake Mtaa wa Unyamwezini, Kata ya Itumbili Wilayani Magu, akiwa ameongozana na Mwanafunzi mwenzie wa miaka hiyo Mzee John Lufega, Dr. Tax baada ya kuona hali ilivyotete katika shule hiyo aliahidi kusaidia ujenzi wa choo shuleni hapo.
Pia amesikitishwa sana kuona vyumba vya madarasa vinane vilivyochakaa na kushindwa kutumika na kupeleka watoto kusoma kwa zamu, Ameahidi pia kufanya ukarabati wa chumba cha darasa alichosomea.
Mkuu wa Wilaya ya Magu ambaye fedha hiyo imetumwa kupitia kwake, akiwa katika kikao cha Wananchi wa Kata Magu mjini na Isandula katika viunga vya shule ya Msingi Nyalikungu, Amempongeza sana na kumshukuru Katibu Mtendaji wa SADC kwa moyo wake na nia yake ya dhati katika kuisadia jamii ya wanamagu wenzake,” Hakika huyu ni Mtu muhimu kwetu tena ni kiongozi mkubwa lakini alisoma hapa Nyalikungu Shule ya msingi na leo bado anaikumbuka shule yake”
“Tunampongeza sana na nitoe wito kwa Wanafunzi wengine waliowahi kusoma hapa nao warudi waje tuifanye shule hii kuwa shule ya mfano na yenye ubora zaidi hata katika taaluma, ili kuvienzi vipaji vya watu waliopata maarifa S/M Nyalikungu maendeleo ni watu na sisi ndiyo tunawajibika kufanya kazi ili kujiletea maendeleo”. Amesisitiza Dkt Sengati.
Wananchi waliofika katika Mkutano huo wa makabidhiano wamemshukuru sana Dr.Tax kwa uzalendo wake, na hata hivyo Mkuu wa Wilaya Dr. Sengati ameamua kumuunga mkono kwa kuendesha harambee ya kuongezea fedha hiyo ili ikidhi kujenga vyumba 12 vya matundu choo, amechangia Tsh. 200,000, Lutengano Mwalwiba DED- Magu amechangia Tsh. 100,000, Afisa Elimu Msingi Tsh. 200,000, Mashaka Mathias Diwani Magu mjini Tsh. 100,000, Velina Emmanuel (Diwani Kata ya Isandula) ametoa tripu 1 ya mchanga, Walimu wote wa Shule msingi Nyalikungu nao wamechangia na wananchi wote ambapo Mheshimiwa DC Sengati ameagiza watendaji wa kata kuratibu fedha hizo zilizochangwa na kuzikabidhi shuleni hapo kwa ajili kazi iliyokusudiwa.
Diwani wa kata ya Magu mjini Mheshimiwa Mashaka Mathias amemshukuru Mheshimiwa DC Sengati kwa uaminifu na uadilifu mkubwa alionao katika kuitumikia wilaya yetu, Pia amesema kwa niaba ya Wanamagu “tunampongeza sana Dr. Tax kwa mchango huu na kwamba tunazitumia fedha hizi kwa kazi iliyokusudiwa”.
Naye Mwalimu Mkuu Beatrice Ngula baada ya kukabidhiwa fedha hizo amewashukuru viongozi kwa mshikamano walio uonyesha katika kusimamia shughuli za maendeleo shuleni hapo, na kwamba wanampongeza sana katibu Mtendaji kwa msaada aliotoa kwa ajili kuisaidia shule ya Nyalikungu ili iendelee kutoa elimu kwa wengine.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa